• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
Beth Mugo apinga uamuzi wa IEBC kutumia KIEMs pekee kuwatambua wapigakura

Beth Mugo apinga uamuzi wa IEBC kutumia KIEMs pekee kuwatambua wapigakura

NA CHARLES WASONGA

SENETA maalum Beth Mugo ndiye mwanasiasa wa hivi punde kupinga uamuzi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwamba ni sajili ya kidijitali pekee itatumika katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Akiongea na wanahabari Jumatatu, afisini mwake katika majengo ya bunge, Nairobi, Bi Mugo alisema matumizi ya mitambo ya kielektroniki, yenye sajili hiyo, pekee kuwatambua wapigakura yatafungia nje idadi kubwa ya wapigakura wenye hitilafu katika alama za vidole.

“Watu wenye hitilafu kwenye alama za vidole kutokana na uzee kama mimi au wale ambao alama hizo zimevurugika kutokana na kazi wanazofanya watafungiwa nje kutekeleza haki yao ya kikatiba endapo sajili mbadala haitatumika,” akasema.

“Jambo kama hili halifai kuruhusiwa. Hii ndio maana kwa niaba ya wazee wenye hitilafu kwenye alama za vidole na watu wengine, naiomba IEBC iruhusu matumizi ya sajili ya daftari kama ilivyokuwa katika chaguzi zilizopita,” Bi Mugo, ambaye ni binamuye Rais Uhuru Kenyatta, akaeleza.

Seneta huyo alimtaka Mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati kutatilisha uamuzi wa tume yake wa kwa itatambua wapiga kura kwa njia ya dijitali pekee.

Kulingana na Bi Mugo, IEBC haijatoa hakikisho kuwa mitambo ya kuwatambua wapiga kura kielektroniki (KIEMs) haitafeli ilivyofanyika katika uchaguzi mkuu wa 2017.

“Bw Chebukati hafai kuwaambia kutoa sababu kwamba sajili za daftari zitatoa nafasi kwa wasimamizi na makarani wa uchaguzi kuendesha udanganyifu kwa kuwapigia kura watu ambao hawatajitokeza. Kauli kama hii haina mashiko na inaashiria kuwa IEBC imewaajiri wasimamizi wa uchaguzi wenye dosari kimaadili,” akaeleza.

Bi Mugo alisema wapigakura wengi haswa walioko katika maeneo ya mashambani watazuiwa kushiriki uchaguzi mkuu wa Agosti 9 endapo IEBC itazingatia matumizi ya mitambo ya KIEMs pekee.

Seneta wa Nandi Samson Cherargei pia alitoa kauli yake kuhusu suala hilo, akitoa wito kwa IEBC kuruhusu matumizi ya sajili zote mbili.

Mkurugenzi wa kampeni za urais za Naibu Rais William Ruto, Gavana Josphat Nanok pia ameunga mkono matumizi ya mifumo hiyo miwili ya kuwatambua wapigakura.

Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya pia umeitaka IEBC kubatilisha uamuzi huo ukisema matumizi ya mitambo ya KIEMs pekee yatanyima idadi kubwa ya wapigakura kushiriki uchaguzi.

Makundi na mashirika ya kijamii tayari yamewasilisha kesi mahakamani kupinga matumizi ya mitambo ya KIEMs pekee katika uchaguzi pekee.

Mapema mwezi huu IEBC ilisema kuwa matumizi ya sajili ya daftari kama njia mbadala ya kuwatambua wapigakura ndio ilitoa mwanya wa udanganyifu katika uchaguzi mkuu wa 2017.

“Utathimini wa uchaguzi mkuu wa 2017 ulionyesha kuwa visa vingi vya udanganyifu vilitokana na matumizi ya sajili za daftari. Tunaamini kuwa matumizi ya sajili za kidijitali yataondoa kutokea kwa maovu hayo ambapo msimamizi wa uchaguzi anafahamu yule ambaye hajapiga kura na nambari yake ya kitambulisho. Msimamizi kama huyo ataweka maelezo ya mpiga kura kama huyo ndani ya mitambo ya Kiems na hivyo kuendeleza uovu huo kwa niaba ya mgombeaji fulani,” Bw Chebukati akasema mnamo Juni 9, 2022 katika ukumbi wa Bomas of Kenya.

  • Tags

You can share this post!

Divock Origi abanduka Liverpool na kuingia katika sajili...

Kenya Kwanza kukagua matumizi ya pesa chini ya utawala wa...

T L