• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Changamoto kwa Sakaja huku muungano wa Azimio ukitawala jiji

Changamoto kwa Sakaja huku muungano wa Azimio ukitawala jiji

NA BENSON MATHEKA

GAVANA ajaye wa Nairobi, Bw Johnson Sakaja, huenda akakabiliwa na kibarua kigumu kufanikisha ajenda yake katika kaunti hiyo baada ya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya kushinda viti vingi katika Bunge la Kaunti ya Nairobi, Seneta na Mwakilishi wa Kike.

Muungano huo ulishinda viti 44 kati ya 85 za uwakilishi wa wadi kaunti ya Nairobi huku chama cha United Democratic Alliance (UDA) na washirika wake katika Kenya Kwanza ukizoa viti 37. Wagombeaji huru walishinda viti viwili.

Kuwepo kwa madiwani wengi wa Azimio katika bunge la kaunti kutamaanisha wanaweza kuzima miswada ya serikali ya Sakaja na kuyumbisha ajenda yake kwa kaunti ya Nairobi.

Bw Sakaja wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa ugavana kwa kupata kura 699,392 dhidi ya mpinzani wake mkuu Bw Polycarp Igathe wa chama cha Jubilee aliyepata kura 576,516.

Katika uchaguzi wa useneta, Bw Edwin Sifuna wa chama cha ODM alipata kura , 716,876 dhidi ya 524,021 za mpinzani wake mkuu Askofu Margaret Wanjiru wa chama cha UDA.

Ushindi wa Bw Sifuna ambaye pia ni wa muungano wa Azimio unamaanisha kuwa uongozi wa Bw Sakaja utapigwa darubini vikali na seneta asiye wa chama chake.

“Inatarajiwa kuwa Bw Sakaja atakuwa na wakati mgumu kufanikisha ajenda zake kwa kuwa juhudi zake zinaweza kuhujumiwa na madiwani wa Azimio walio wengi huku matumizi ya pesa za kaunti yakipigwa darubini na seneta ambaye pia ni wa muungano huo,” asema mchanganuzi wa siasa za Nairobi Faustine Abijo.

Kati ya madiwani 44 wa Azimio kaunti ya Nairobi 35 ni wa ODM, 5 ni wa chama cha Wiper na 4 ni wa chama cha Jubilee.

Kulingana na matokeo yaliyotangazwa na Afisa wa IEBC kaunti ya Nairobi Bw Albert Gogo, Bi Esther Passaris wa ODM alishinda kiti cha Mwakilishi wa wanawake kwa kura 698,929 dhidi ya 586,246 za Millicent Omanga wa UDA.

Katika uchaguzi wa ubunge, Azimio La Umoja One Kenya ilipata wabunge wengi kaunti ya Nairobi wakiwemo Babu Owino – ODM (Embakasi East), Jalang’o – ODM (Lang’ata), Tim Wanyonyi – ODM (Westlands), Mark Mwenje – Jubilee (Embakasi West), Amos Mwago – Jubilee (Starehe), Beatrice Elachi – ODM (Dagoretti North), Yusuf Hassan – Jubilee (Kamukunji), George Aladwa – ODM (Makadara), Tom Kajwang’ – ODM (Ruaraka) na Antony Oluoch – ODM (Mathare), Julius Mawathe – Wiper (Embakasi South), na Mwalimu Peter Orero – ODM (Kibra).

Wabunge wa Kenya Kwanza jijini ni Benjamin Gathiru – UDA (Embakasi Central), Mwafrika Augustine Kamande – UDA (Roysambu), James Gakuya (Embakasi North) – UDA na John Kiarie – UDA (Dagoretti South).

  • Tags

You can share this post!

Wagombeaji wa DAP-K walaumu Oparanya kwa kushindwa

Barasa kortini kudai fidia baada ya IEBC kuahirisha uchaguzi

T L