• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Wagombeaji wa DAP-K walaumu Oparanya kwa kushindwa

Wagombeaji wa DAP-K walaumu Oparanya kwa kushindwa

NA SHABAN MAKOKHA

MIZOZO ya ndani iliyoshuhudiwa katika muungano wa Azimio wakati wa kampeni inaendelea hata baada ya uchaguzi huku wagombeaji wa chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) wakilaumu uongozi wa ODM eneo la Magharibi kwa kuhujumu ushindi wao kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Wagombeaji wa viti mbali mbali kwa tiketi ya DAP- Kenya katika kaunti ya Kakamega sasa wanalaumu Gavana Wycliffe Oparanya kwa kuwanyima ushindi huku akitia nguvu chama chake aweze kuwa Waziri wa Fedha iwapo kiongozi wa ODM Raila Odinga atashinda urais.

Katika eneo bunge la Butere, wagombeaji wote wa viti vya MCA kwa tiketi ya DAP- K waliibuka katika nafasi ya pili nyuma ya wale wa ODM.

Wanadai kwamba Bw Oparanya alitumia uwezo wake wa kifedha na ushawishi wake wa kisiasa kuhakikisha ODM ilishinda viti vingi kwenye uchaguzi uliopita.

Bw Thomas Maseno Wanga aliyeshindwa na Philip Maina katika wadi ya Marama Central na Geoffrey Opete Aswani aliyeshindwa katika wadi ya Butsotso South wameapa kuchukua hatua za kisheria kupinga matokeo ya uchaguzi.

Bw Wanga alidai kwamba alipokonywa haki yake ya kidemokrasia ya kushinda na kuwa diwani wa wadi ya Marama Central kupitia ushawishi wa Bw Oparanya aliyemlaumu kwa kuhonga wapigakura tarehe ya uchaguzi ili kumhakikishia ushindi Bw Maina wa ODM.

“Tuko na ushahidi wa yaliyotendeka siku ya uchaguzi na kabla ya siku hiyo. Kabla ya siku ya kura, walinunua vitambulisho vya wapigakura katika ngome zetu, siku ya uchaguzi, waliwatisha maajenti wetu na kuwafukuza baadhi yao kutoka vituo vya kupiga kura,” alidai Bw Wanga.

  • Tags

You can share this post!

Brentford yadhalilisha Manchester United katika EPL

Changamoto kwa Sakaja huku muungano wa Azimio ukitawala jiji

T L