• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:55 AM
Chap Chap hatutamezwa na UDA – Mbunge

Chap Chap hatutamezwa na UDA – Mbunge

NA PIUS MAUNDU

MBUNGE wa Kibwezi Magharibi, Mwengi Mutuse amemsuta Kaimu Katibu Mkuu wa United Democratic Alliance (UDA) Cleophas Malala kuhusu shinikizo lake kwa vyama tanzu vya Kenya Kwanza Alliance kuvunjwa na kujiunga na UDA.

Mbunge huyo aliyechaguliwa kupitia tiketi ya Maendeleo Chap Chap (Mccp) alimshutumu Bw Malala kwa kufanya kazi na muungano wa Azimio ili kusababisha misukosuko katika kambi ya Rais William Ruto kutoka ndani.

“Juzi tulisikia watu fulani wakisema kuwa watamhujumu Rais Ruto kutoka ndani na nje. Tutawataja mafuko kwa majina yao. Bw Malala wewe mtatizaji. Mambo unayoyafanya ni sawia na hujuma. Unamhujumu Rais,” alisema Bw Mutuse.

Mbunge huyo alizungumza Jumatatu mjini Makindu Kaunti ya Makueni alipokuwa akipatiana Sh53 milioni za basari kwa wanafunzi wa vyuo na sekondari.

Alisisitiza kuwa chama cha Maendeleo Chap Chap kitamkaidi Bw Malala.

“Kama kiongozi niliyechaguliwa kwa tiketi ya Mccp na ijulikane kuwa chama hiki hakitavunjwa. Badala yake, tutakieneza kote nchini ili kiwe imara kabla ya chaguzi za 2027,” alisema.

Mnamo wikendi, Bw Malala alieleza maafisa wakuu wa serikali katika utawala wa Kenya Kwanza ambao bado wanakwamilia vyama vyao kuchagua kati ya kuwepo serikalini au kujiuzulu nyadhifa zao na kung’ang’ania vyama vyao vya kisiasa.

“Haina maana kuwa waziri na bado unashikilia chama chako,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

Maxine Wahome kupimwa akili Mathari kabla ya kujibu shtaka...

SHINA LA UHAI: Matibabu ya kansa nchini yamletea afueni...

T L