• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 1:14 PM
Chebukati atauma Ruto?

Chebukati atauma Ruto?

WANDERI KAMAU na DERICK LUVEGA

NAIBU Rais William Ruto ameendelea kupuuza amri ya mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Bw Wafula Chebukati ya kuwazuia wanasiasa kutoshiriki kwenye hafla zozote za kuchangisha pesa kuanzia Desemba 9.

Licha ya agizo hilo, Dkt Ruto amekuwa akitoa michango ya mamilioni ya pesa kwenye mikutano yake kwa makundi mbalimbali kama ambavyo imekuwa kawaida yake.

Hii ni licha ya tarehe ya mwisho iliyotangazwa na IEBC ambapo wanaopania kuwania vyeo vya kisiasa kwenye uchaguzi mkuu ujao wangesitisha mikutano yao ya harambee kupita.

Kwenye ziara ambayo amekuwa akifanya katika eneo la Magharibi mwa Kenya kuanzia Jumatano, Dkt Ruto amekuwa akitoa michango ya maelfu ya pesa kwa wafuasi wake, akisema “analenga kuwasaidia kujiinua kiuchumi.”

Jumatano, Dkt Ruto alitoa mchango wa Sh500,000 kuwasaidia wafanyabiashara katika eneo la Butali, Kaunti ya Kakamega.

Na jana Alhamisi, aligawa Sh500,000 katika soko la Eshibiya, Kaunti ya Vihiga kuwasaidia wafanyabiashara.

Alitoa kiasi kama hicho katika eneo la Ebukanga “kuwainua kiuchumi” wenyeji.

Vile vile, alitoa Sh20,000 katika maeneo ya Mahanga na Majenyi kama “zawadi” kwa vijana.

Hata hivyo, Dkt Ruto alionekana kubadilisha mbinu yake ya awali, ambapo badala ya kutoa michango hiyo kama pesa taslimu, alisema “zingewasilishwa na mtu wake.”

Wafanyabiashara waliozungumza na ‘Taifa Leo’ katika eneo la Butali walisema, fedha hizo ziliwasilishwa na mtu aliyekuwa ajenti wa Dkt Ruto.

Alhamisi, mbunge Rigathi Gachagua (Mathira) pia aliongoza hafla ya kuchangisha pesa kuwasaidia zaidi ya wahudumu 1,500 wa bodaboda katika Uwanja wa Ruring’u, Kaunti ya Nyeri.

Ingawa haikubainika wazi kiwango cha pesa kilichochangwa, mbunge huyo alisema mchango huo unafuatia “ombi ambalo wahudumu hao waliwasilisha” kwa Dkt Ruto.

Wadadisi wanasema hatua hiyo ni kukaidi sheria za uchaguzi, ikizingatiwa kuwa Bw Chebukati alipiga marufuku wanasiasa kushiriki kwenye michango yoyote ya pesa.

Bw Chebukati alitoa agizo hilo Jumatano wiki iliyopita, alipofanya kikao na Kamati ya Seneti kuhusu Sheria na Haki kwa njia ya mtandao.

“Hili si agizo letu bali ni hitaji la kisheria. Wawaniaji wa nyadhifa za kisiasa wamezuiwa kushiriki kwenye michango yoyote ya pesa miezi minane kabla ya uchaguzi huo,” akasema Bw Chebukati.

Mwenyekiti huyo alisema mwanasiasa ama mgombeaji yeyote atakayepatikana akikiuka agizo hilo atazuiwa kushiriki kwenye uchaguzi huo.

Hata hivyo, wadadisi wanasema ingawa juhudi za Bw Chebukati zinalenga kudumisha uwajibikaji katika siasa, itakuwa vigumu kwake kutekeleza agizo hilo.

“Huenda agizo hilo likakosa makali yoyote kwa kuwa hana uwezo kumfuatilia kila mwanasiasa. Isitoshe, Katiba i wazi kwamba mtu hawezi kuzuiwa kushiriki kwenye michango ikiwa hajashtakiwa kwenye mahakama na taratibu zote za kisheria kufuatwa. Ni mtihani mgumu,” akasema Prof Macharia Munene, ambaye ni mchanganuzi wa siasa kwenye mahojiano.

Bw Felix Onyango, ambaye pia ni mdadisi wa siasa, anataja agizo la Bw Chebukati kama mlima mrefu ambao huenda akashindwa kuukwea.

“Baadhi ya wanasiasa ambao Bw Chebukati anakabiliana nao wametumia mbinu hiyo kujijenga tangu utawala wa Kanu. Ni kama kumwambia mtu aliyelelewa na maziwa kumwambia kuacha kuyanywa akiwa mtu mzima. Ni vigumu. Anahitaji uungwaji mkono wa asasi nyingine za serikali, hasa mahakama, ili kufaulu,” akasema Bw Onyango.

Wadadisi wanasema wanasiasa ni viumbe wajanja, ambao watabuni mbili mbadala kuhujumu agizo la Bw Chebukati.

“Bila kujali mrengo wao wa kisiasa, watalazimika kubadil mbinu japo lazima wahakikishe ndio waliotoa fedha kwa makundi yanayolengwa,” akaeleza Bw Onyango.

You can share this post!

Njuki tayari kuingia kambi ya Ruto lakini kwa masharti

Mashabiki waliopokea chanjo na ambao hawana virusi ndio wa...

T L