• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:15 PM
Njuki tayari kuingia kambi ya Ruto lakini kwa masharti

Njuki tayari kuingia kambi ya Ruto lakini kwa masharti

Na ALEX NJERU

GAVANA wa Tharaka Nithi Muthomi Njuki amesema yuko tayari kujiunga na mrengo wa Naibu Rais William Ruto lakini kwa masharti fulani.

Akiongea alipotoa hotuba kuhusu Hali ya Kaunti hiyo mjini Kathwana Jumatano, Bw Njuki ambaye awali alikuwa ametangaza kumuunga mkono kiongozi wa ODM Raila Odinga, alisema bado anafanya mashauriano kabla ya kufanya uamuzi huo.

“Nimefanya mashauriano na ningali nafanya mashauriano kuhusu suala hili muhimu. Hata hivyo, nawalaumu wanasiasa wa hapa kwetu kwa kuunga Ruto mkono bila kuuliza jinsi watu wetu watafaidika akishinda,” akasema Bw Njuki.

Gavana huyo alisema hatatangaza kuwa anaunga mkono azma ya urais ya Dk Ruto bila makubaliano kuhusu manufaa ambayo wakazi wa Tharaka Nithi watapata akiingia Ikulu.

Bw Njuki alisema eneo hilo limesalia nyuma kimaendeleo kwa sababu wanasiasa wamekuwa wakiwaunga mkono wagombeaji urais bila kukubaliana kuhusu “yale watu wetu watapata.”

Mshirika wa Njuki, Mbunge wa Maara Kareke Mbiuki, amekariri mara kadha kwamba Gavana huyo atatetea kiti chake kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Mnamo Jumatano Bw Njuki alimwambia Mbiuki hivi; “Nenda ukamwambie rafiki yako Naibu Rais Dkt Ruto kwamba niko tayari kwa ndoa lakini sharti tuchumbiane na kujadiliane.”

Gavana Njuki amewalaki kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na kiongozi wa ODM Raila Odinga walipozuru Tharaka Nithi kuvumisha azma zao za urais lakini alimkwepa Dkt Ruto alipozuru eneo hilo juzi.

Hata hivyo, licha ya Seneta Kithure Kindiki na wanasiasa wengine kushambulia Bw Njuki katika mikutano ya hadhara, Dkt Ruto amekuwa akimsihi gavana huyo, kwa upole, akubali kufanya kazi naye.

You can share this post!

Serikali ifadhili elimu ya juu ya madaktari – CoG

Chebukati atauma Ruto?

T L