• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Diwani maalum wa ODM Solomon Ngugi aapishwa Mombasa

Diwani maalum wa ODM Solomon Ngugi aapishwa Mombasa

Na WINNIE ATIENO

BUNGE la Kaunti ya Mombasa limemwapisha Bw Solomon Ngugi kuchukua nafasi ya aliyekuwa diwani maalumu Mohamed Hatimy, ambaye aliaga dunia Novemba 2020.

Bw Hatimy ambaye alikuwa mmoja wa wanachama sugu wa ODM katika Kaunti ya Mombasa alifariki baada ya kuugua Covid-19.

Bw Ngugi ambaye anafahamika kuwa miongoni mwa wanachama wa ODM wanaotegemewa katika shughuli za kuvumisha chama hicho mashinani, ameahidi kuendelea kuwa mwaminifu kwa chama hicho baada ya kuapishwa Jumanne.

“Ninakishukuru chama cha ODM kwa uteuzi huu. Naomba madiwani wenzangu wanilinde na wanishike mkono katika safari hii,” aliambia Taifa Leo punde baada ya kuapishwa.

Madiwani wa chama hicho ambao ndio wengi katika bunge hilo la kaunti, walimshauri awe mwaminifu kwa kiongozi wa chama Raila Odinga na naibu wake Hassan Joho aliye pia Gavana wa Kaunti ya Mombasa.

Kiranja wa walio wengi katika bunge hilo la kaunti, Bw Junior Wambua, alisema Bw Ngugi alituzwa kwa kutumikia chama cha ODM kwa uaminifu kwa miaka mingi.

“Tunamkaribisha bungeni, aendelee kutumikia wananchi. Bunge letu liko imara,” alisema Bw Wambua.

Naye Spika Aharub Khatri aliwataka viongozi kujitolea mhanga kupigania maslahi ya wananchi.

“Msiangalie matumbo yenu kwani wananchi wana mahitaji yao na ni jukumu letu kuyatimiza. Bw Ngugi ameapishwa tayari. Atashughulikia sana maslahi ya watu wanaoishi na ulemavu,” alisema.

Seneta wa Mombasa, Bw Mohamed Faki aliwataka madiwani hao kuvumisha sifa za chama hicho mashinani wakati Wakenya wanapojiandaa kushiriki uchaguzi mkuu mwaka 2022.

“Kifo cha Bw Hatimy kilikuwa pigo kubwa sana kwa chama cha ODM Kaunti ya Mombasa. Bw Ngugi amechukua nafasi kubwa sana na tunatarajia kwamba ‘utatekeleza wajibu wako kulingana na sera za chama na pia maslahi ya wakazi wa Mombasa’,” alisema Seneta Faki.

You can share this post!

NGILA: Tuwazie upya kuhusu Afrika tunayoitamani kiteknolojia

Virgil van Djik tayari kurejea uwanjani – Jurgen Klopp