• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
NGILA: Tuwazie upya kuhusu Afrika tunayoitamani kiteknolojia

NGILA: Tuwazie upya kuhusu Afrika tunayoitamani kiteknolojia

Na FAUSTINE NGILA

JUMATATU wiki hii niliongoza kikao kuhusu jinsi mataifa ya Afrika yanajiandaa kwa Mapinduzi ya Nne ya Viwanda ambapo niliwahoji magwiji wa uchumi wa dijitali barani.

Mwanzo, ukosefu wa usawa katika masuala yote ya kidijitali ulijitokeza kama kisiki kikuu katika azma ya Afrika kujiendeleza katika dunia ya sasa.

Ni wazi kuwa wananchi wa mashinani, wanawake na watu wa pato la chini tayari wameachwa nyuma katika matumizi ya teknolojia za kisasa ambazo zimesaidia pakubwa kusuluhisha baadhi ya changamoto barani.

Ni bayana kuwa mataifa mengi yanazidi kujikokota kubuni sheria na kanuni za kuboresha utendakazi wa teknolojia. Je, ni nini tunafanya kama bara kupata mgao wa maana katika uchumi wa dijitali duniani?

Afrika, iliibuka, ina fursa ya mwaka kuchangamkia maendeleo ya mageuzi ya viwanda ya sasa iwapo haitaki kuachwa nyuma tena na mabara mengine kama Amerika, Uropa na Asia kama ilivyofanyika miaka ya tisini.

Lakini ili kuweza kufika hapo, wadau walikubaliana kuwa viongozi wa bara hili wanahitaji kubadilisha fikra zao kwanza, hasa kwa kutengea masuala ya teknolojia na ubunifu fedha za kutosha pamoja na kufanya kampeni za kuhamasisha umma kuhusu umuhimu wa Mapinduzi ya Nne ya Viwanda.

Pia, ili kujiunga na mataifa yalioyoendelea katika ulingo huu, mataifa yote 55 ya Afrika, ingawa yana sheria mbalimbali, yanafaa kukubaliana kuhusu kupunguza bei ya intaneti na pia kuondoa ushuru wa simu za kisasa ambazo zinatumika katika utoaji wa huduma ainati za kiteknolojia.

Sekta za elimu, afya, uchukuzi, sheria na kilimo tayari zimebadilishwa pakubwa na matumizi ya program za simu lakini bei ghali ya vifaa na intaneti inazidi kuwafungia nje mamilioni ya Waafrika ambao sasa hawawezi kufurahia huduma hizi.

Hii inamaaniosha kuwa, badala ya mageuzi ya teknolojia kuwahusisha watu wote, yanabagua watu kwa msingi wa mapato ya kifedha kwa sababu serikali za mataifa ya Afrika zimefumbia macho suala muhimu kuhusu kupunguza gharama ya kutumia mitandao.

Lingine ni kuhusu mpango mzima wa Umoja wa Afrika (AU) kutumia mradi wake wa soko huru barani kuhakikisha watu wa mataifa mbalimbali wamefanya biashara bila vikwazo, hasa mitandaoni.

Ingawa changamoto tayari ni nyingi, bado kuna nafasi wa marais wa mataifa haya kukubaliana kufungua mipaka yao kwa biashara ili Afrika ipate usemi wa maana katika soko la dunia.

Iwapo Afrika itafaulu kuunganisha mataifa yake yote kuwa soko moja, basi tunakuwa na soko la watu bilioni 1.2 kama Uchina na India, na tutaipiku Amerika ambayo ina watu milioni 300.

Ushawishi tutakuwa tumepata na utatuwezesha kusikizwa na pande zingine za dunia wakati ambapo tuna jambo la kusema. Kwa mfano, data ya Afrika imekuwa ikitumiwa kiholea bila kujali lakini tukiwa na ushawishi huu mataifa yaliyoendelea yatatukoma.

Hata hivyo, kila Mwafrika, popote alipo hata ughaibuni, anafaa kufikiria upya na kubadilisha matazamo wake kuhusu mwelekeo wa bara hili katika kipindi hiki cha teknolojia, la sivyo tutaachwa nyuma tena na kuendelea kuwa watumizi wa teknolojia badala ya wavumbuzi.

You can share this post!

ONYANGO: Vyama vya kikabila si kichocheo cha maendeleo

Diwani maalum wa ODM Solomon Ngugi aapishwa Mombasa