• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
EACC yashinikizwa ifuatilie matamshi ya Ruto kuhusu Wamalwa

EACC yashinikizwa ifuatilie matamshi ya Ruto kuhusu Wamalwa

NA TITUS OMINDE

VIONGOZI kutoka Jamii ya Waluhya wanataka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imtangaze Naibu Rais William Ruto kama mmoja wa wanasiasa wasio na maadili, kutokana na matamshi yake ya hivi majuzi ya kumtaja waziri wa ulinzi Eugene Wamalwa kama mwanamke.

Wakiongozwa na Mbunge wa Lugari, Bw Ayub Savula, walimtaja Dkt Ruto kama kiongozi ambaye anaweza kuhatarisha uhusiano kati ya jamii za humu nchini na pia kuhatarisha uhusiano wa kimataifa.

Bw Savula alitoa changamoto kwa EACC sio tu kuzingatia ufisadi pekee bali pia masuala ya maadili na uadilifu miongoni mwa wanasiasa wanapohutubia mikutano ya kisiasa.

Alisikitika kwamba matamshi kama hayo si tu kinyume cha maadili bali yanadhoofisha maadili miongoni mwa watoto wanaoheshimu viongozi wa aina ya Dkt Ruto.

Akizungumza katika soko la Mbururu Kaunti Ndogo ya Likuyani Jumapili, Bw Savula alitoa changamoto kwa Dkt Ruto kuacha kiburi na kuomba msamaha kwa familia ya Bw Wamalwa na jamii ya Waluhya kwa jumla.

“Familia ya Bw Wamalwa na jamii ya Waluhya kwa jumla inataka heshima. Bw Ruto lazima afanye jambo la heshima na kuomba msamaha kwa matamshi hayo yasiyokuwa na maadili,” akasema Bw Savula.

Akizungumza wakati wa kampeni zake za ugavana Kakamega, Bw Savula alionya kuwa ikiwa Bw Ruto hataomba msamaha kwa jamii ya Walya ataongoza maandamano dhidi ya Bw Ruto.

“Iwapo Ruto atakosa kuomba msamaha ndani ya siku saba, nitaongoza maandamano ya amani dhidi yake katika eneo la Magharibi mwa Kenya ili ulimwengu ujue kiongozi huyo hana maadili,” Bw Savula alisema.

Bw Savula alijuta kuwa “Ruto ambaye anadai kuwa Mkristo aliyezaliwa mara ya pili anatoa matamshi ya ovyo hadharani kutokana na tabia yake ya hasira na pupa ya kutaka kuongoza Wakenya kwa lazima.”

Alisema kuwa Wakenya tayari wameona tabia halisi ya Bw Ruto ambaye anataka kuongoza Nchi na hana heshima kwa viongozi wengine na jamii nyingine.

“Ilikuwa bahati mbaya kwa mtu anayetaka kuongoza nchi kutoheshimu jamii nzima. Bw Ruto ni mtu aliyejawa na hasira na akipewa nafasi ya kuongoza nchi hii hasira yake itaharibu umoja wa Wakenya,” akaongeza Bw Savula.

Wiki moja iliyopita Bw Ruto alipokuwa akihutubia mikutano ya hadhara magharibi mwa Kenya alisema kuwa mila za jamii ya Kalenjin haziruhusu mwanamume kumpiga mwanamke kofi, matamshi aliyotoa akimrejelea Eugene Wamalwa.

  • Tags

You can share this post!

Raila ‘aoshwa laana ya 1969’

Balala abururwa hadi kortini kwa madai ya ufisadi

T L