• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Raila ‘aoshwa laana ya 1969’

Raila ‘aoshwa laana ya 1969’

NA WANDERI KAMAU

MWANIAJI urais wa muungano wa Azimio-One Kenya, Bw Raila Odinga, amepata mpenyo mkubwa wa kisiasa katika eneo la Mlima Kenya, baada ya wazee wa jamii ya Agikuyu kuondoa masharti ya kiapo kilichoizuia jamii hiyo kumpigia kura mwaniaji urais kutoka jamii nyingine.

Jamii hiyo ilipewa kiapo hicho mnamo 1969, nyumbani kwa rais wa kwanza Mzee Jomo Kenyatta katika kijiji cha Ichaweri, eneo la Gatundu, Kaunti ya Kiambu.

Watu wengi waliopewa kiapo hicho ni wale walioshiriki kwenye vita vya Mau Mau.

Kulingana na masharti ya kiapo hicho, jamii hiyo haikupaswa kumpigia kura mtu yeyote kutoka nje ya Mlima Kenya hasa kutoka jamii ya Waluo.

Vile vile, kiapo hicho kilisema uongozi wa Mlima Kenya kamwe haungetoka mashariki mwa Mto Chania, hilo likimaanisha hakuna kiongozi yeyote kutoka eneo hilo angetoka kutoka kaunti za Nyeri, Murang’a, Kirinyaga, Tharaka Nithi Embu ama Meru, hivyo urais ungebaki Kiambu pekee

Kwenye kiapo hicho wenyeji walionywa kwamba wangepatwa na laana ikiwa wangekiuka sharti lolote la kiapo hicho.

Hata hivyo, huenda hali ya kisiasa katika eneo hilo ikabadilika, baada ya wazee wa Kiama Kia Ma (Chama Cha Ukweli), kufanya tambiko maalum katika eneo la Kiambaa, Kaunti ya Kiambu, kufutilia mbali masharti ya kiapo hicho.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo jana Jumatatu, mwenyekiti wa chama hicho Ngungu Gaithuma alisema masharti hayo yamekuwa yakiifunga jamii hiyo kisiasa.

“Lengo la tambiko letu ni kuiunganisha jamii. Baadhi ya masharti yaliyokuwa kwenye kiapo hicho ni ya kuleta migawanyiko badala ya kuiunganisha jamii na Wakenya wote kwa jumla. Kuna kosa lipi kiongozi kuchaguliwa kutoka pahali popote nchini ikiwa ana uwezo wa kuwaongoza raia?” akashangaa Bw Gaithuma, akitaja baadhi ya masharti hayo kama yaliyopitwa na wakati.

VITISHO VYA KIAPO

Alisema mchakato huo wa kuondoa laana hiyo uliwahusisha wazee zaidi ya 20 wenye umri wa kati ya miaka 65 na zaidi walioshiriki kwenye kiapo hicho.

Bw Gaithuma alipuuza baadhi ya vitisho vya masharti hayo kama vile kuleta “laana dhidi ya wenyeji”, akieleza kuwa licha ya onyo hilo, walimchagua Mwai Kibaki mnamo 2002 kuwa rais bila kukumbwa na mkosi wowote.

Marehemu Kibaki alitoka katika Kaunti ya Nyeri, ikiwa miongoni mwa zile zilitajwa na kiapo hicho kuwa hakuna kiongozi ambaye angetoka huko.

Kulingana na wadadisi wa siasa, kuondolewa kwa masharti hayo ni afueni kubwa kwa Bw Odinga, kwani “kunaifungua” jamii hiyo dhidi ya baadhi ya masharti iliyokuwa imepewa dhidi ya kumchagua kiongozi yeyote kutoka jamii ya Waluo.

“Msingi wa kiapo hicho ulitokana na uhasama mkubwa uliokuwepo kati ya Mzee Kenyatta na babake Bw Odinga, Jaramogi Oginga Odinga. Hivyo, msukumo wake ulitokana na hasira alizokuwa nazo Mzee Kenyatta dhidi ya Jaramogi, wala si uhasama wa kisiasa kati ya jamii ya Agikuyu na Waluo,” akasema Prof Macharia Munene, ambaye ni mdasisi wa siasa na mhadhiri wa Historia.

Tangu kubuni handisheki na Bw Odinga mnamo 2018, Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akieleza angependelea Bw Odinga kuwa mrithi wake baada ya kung’atuka uongozini mwezi ujao.

Kando na hayo, jumbe za wazee kutoka jamii hizo mbili zimekuwa zikifanya vikao katika maeneo ya Mlima Kenya na Nyanza “kurejesha urafiki” kati yazo.

Kwa mara ya kwanza wiki iliyopita, Rais Kenyatta alimfanyia kampeni Bw Odinga katika kaunti za Nairobi, Laikipia na Samburu, akimtaja kuwa kiongozi bora ikilinganishwa na mpinzani wake mkuu, Naibu Rais William Ruto.

  • Tags

You can share this post!

Umaarufu wa Kidero tishio kwa ubabe wa ODM Nyanza

EACC yashinikizwa ifuatilie matamshi ya Ruto kuhusu Wamalwa

T L