• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Elachi atunukiwa Unaibu Waziri Uhuru akipanua serikali yake

Elachi atunukiwa Unaibu Waziri Uhuru akipanua serikali yake

Na COLLINS OMULO

Aliyekuwa Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi amejiunga na serikali ya Rais Uhuru Kenyatta baada ya kuteuliwa waziri msaidizi.

Kupitia tangazo katika Gazeti rasmi la serikali, Rais Kenyatta alimteua Bi Elachi waziri msaidizi katika Wizara ya Utumishi wa Umma na masuala ya jinsia.

Bi Elachi alijiuzulu kama spika wa bunge la kaunti ya Nairobi Agosti mwaka jana baada ya kutofautiana vikali na aliyekuwa gavana wa kaunti hiyo Mike Sonko na madiwani kadhaa.

Ingawa jina lake halikuwa katika uteuzi ambao Rais Kenyatta alitangaza Jumatano, alikuwa miongoni mwa mawaziri wasaidizi wanane walioapishwa katika Ikulu ya Nairobi.

Hafla hiyo iliongozwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua.Miongoni mwa walioapishwa kuwa mawaziri wasaidizi ni Bw Eric Simiyu Wafukho ( Wizara ya Fedha), Jackson Musyoka Kalla (Wizara ya Leba), Lawrence Angolo Omuhaka (Wizara ya Kilimo) na Profesa Japheth Ntiba Micheni ( idara ya haki katika ofisi ya mwanasheria mkuu).

Wengine ni aliyekuwa kiongozi wa wanafunzi katika chuo kikuu cha Nairobi David Osiany (wizara ya viwanda na biashara) DktSara Ruto (Elimu), Zachary Ayieko (Kawi ) and Bw Alex Mburi Mwiru (Ardhi na Mipango ya miji).

Akiwahutubia baada ya kuapishwa, Rais Uhuru Kenyatta aliwataka wahakikishe miradi ya serikali inayotekelezwa na wizara zao imekamilika.Rais aliwataka washirikiane katika kufanikisha ajenda ya serikali.

“Tuko na jukumu kubwa mbele yetu, jukumu la kukamilisha miradi na mipango ambayo tumeanzisha. Natarajia kuona mchango wenu katika kuikamilisha,” alisema.

Mnamo Agosti 2020, Elachi alishangaza nchi alipowasilisha barua ya kujiuzulu kama spika wa bunge la kaunti ya Nairobi kwa Rais Uhuru Kenyatta baada ya mzozo uliogawanya madiwani kwa mirengo miwili baadhi wakimuunga mkono na wengi wakipinga uongozi wake.

Alipojiuzulu ghafla, Elachi alitaja vitisho katika maisha yake na familia yake kama sababu za kuacha wadhifa wa spika wa bunge la kaunti ya Nairobi.

Pia alilaumu vita vya ubabe, hujuma na Bw Sonko kuingilia majukumu yake kama sababu ya kujiuzulu.Hata hivyo, baadhi ya madiwani walikuwa wakipanga kuwasilisha mswada wa kumuondoa ofisini wakati alipojiuzulu.

“Gavana Sonko, hauwezi kuendelea kutisha maisha ya watu na familia zao. Una familia pia. Hauwezi kuwa na kila kitu. Linda kile ambacho Mungu amekupatia,” alisema kwenye barua yake ya kujiuzulu.

Elachi alikuwa amerejea ofisini Oktoba 2019 zaidi ya mwaka mmoja kufuatia kuondolewa ofisini na madiwani Septemba 2018.Mwanasiasa huyo ana uhusiano wa muda mrefu wa kisiasa na Rais Kenyatta na chama cha Jubilee.

Alitumia tiketi ya chama hichi kugombea kiti cha ubunge cha Dagoreti Kaskazini kwenye uchaguzi mkuu wa 2017 lakini akashindwa na Simba Arati wa chama cha ODM.Kabla ya kugombea kiti hicho alikuwa kiranja wa wengi katika seneti.

You can share this post!

Jubilee yawaonya vikali madiwani wa ngome ya Ruto...

MWANAUME KAMILI: Haiwezekani kushiriki uovu ukaepuka dosari!