• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 5:06 PM
Enzi ya Dkt Ruto yaashiria mwanzo mpya kwa wakazi wa Mlima Kenya

Enzi ya Dkt Ruto yaashiria mwanzo mpya kwa wakazi wa Mlima Kenya

NA RICHARD MUNGUTI

KUAPISHWA kwa Dkt William Samoei Ruto kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Kenya kunaashiria mwanzo mpya kwa eneo la Mlima Kenya ambalo halijui litakalojiri kabla ya mwaka wa 2027, uchaguzi mkuu mwingine utakapofanywa.

Kwa eneo hili kumchagua Dkt Ruto ni sawa na kucheza karata ya pata potea lakini waliojitokeza kumpa kura wakiamini atatekeleza ahadi za wakati wa kampeni.

Huu ndio wakati wa kwanza kwa eneo hili kuanza utawala mpya wa kisiasa katika mwongozo na mazingira ya utaifa kinyume na hapo awali lilipoegemea uongozi uliojengwa chini ya mizizi ya “mtu wa nyumba.”

Wachaganuzi mbalimbali wa masuala ya kisiasa wameeleza misimamo mbalimbali jinsi eneo hilo lililo na idadi kubwa ya wapigakura litakavyojimudu kisiasa na kiuchumi chini ya utawala wa mtu kutoka nje ya eneo lenyewe.

Wanaounga mkono mabadiliko wako na ushauri muwafaka kwa utawala wa Dkt Ruto ilhali walio na maoni tofauti wanahisi hatatekeleza ahadi zake kwa wakazi wa eneo hili.

Wakati nchi hii ilipokuwa inapambana na walowezi wa kikoloni, eneo la Mlima Kenya liliwategemea viongozi kama vile marehemu Dedan Kimathi kabla ya hayati Mzee Jomo Kenyatta kutwaa hatamu za uongozi.

Baada ya eneo la Mlima kutengwa katika kile kilichochukuliwa kuwa uongozi wa kiimla kati ya 1978-2002 chini ya utawala wa hayati Daniel arap Moi aliyetwaa usukani kutoka kwa hayati Kenyatta, eneo hili halijaruhusu uongozi wa “mgeni” ndipo likazindua kampeni za kumng’oa Moi mamlakani.

Eneo hilo liliungana kumchagua mmoja wao kutwaa hatamu za uongozi baada ya Moi.

Kutoka 1992 hadi 2017, eneo kilo limempigia kura mmoja wao kuwa rais.

Ni katika muktadha huu hilo eneo limeonyesha imani na kumthamini “mgeni” kuongoza wakiwa na matumaini atalistawisha kiuchumi na hasa wakiashiria kutakuwa na uhuru wa kibiashara.

Eneo hilo liko na matumaini halitasononeka chini ya utawala wa Dkt Ruto.

Lakini ikitokea kwamba wakazi hawataridhika na uongozi wa sasa bila shaka litaanza kusaka uungwaji mkono na miungano ya kisiasa katika jitihada za kutafuta urais wakati wa uchaguzi mkuu wa 2027.

Ingawa hivyo, Dkt Ruto alifaulu kuwaridhisha wakazi wa eneo la Mlima Kenya kwamba atawafaidi katika masuala mbalimbali haswa ya kibiashara na kilimo ndipo wakapiga kura asilimia 42 katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Wakazi wa Mlima Kenya walikubali kukipigia chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Dkt Ruto na kuwaacha wengi vinywa wazi kwa mshangao. Aidha, kwa mara ya kwanza walikataa ushauri wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta wa kumuunga mkono kinara wa Azimio Raila Odinga na naibu wake Bi Martha Karua aliotazamia wangemrithi.

“Mambo ni sawa, niulizeni mie. Tuko salama katika uongozi wa Dkt Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua. Mlima Kenya hauna shida kuungana. Kile tunahitaji sasa ni umoja wa kitaifa ili tujenge Kenya,” amesema aliyekuwa Mkuu wa Mkoa Joseph Kaguthi anayejivunia kufanyia kazi nyakati za ukoloni hadi utawala wa Bw Uhuru Kenyatta.

  • Tags

You can share this post!

Rais Ruto kuwateua haraka iwezekanavyo majaji sita...

Wapenzi washtakiwa kwa kumtesa mtoto

T L