• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:07 PM
Gachagua alipua vinyonga wa Azimio

Gachagua alipua vinyonga wa Azimio

NA WANDERI KAMAU

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amewaonya wanasiasa waasi wanaohama kutoka mrengo wa Azimio la Umoja na kujiunga na serikali ya Kenya Kwanza dhidi ya kuitisha teuzi kuu serikalini kwani “wana hisa chache katika utawala huo”.

Bw Gachagua aliufananisha utawala wa Rais William Ruto na kampuni, ambapo wenye hisa nyingi ndio hunufaika kwanza.

“Hii serikali ni kampuni na ina hisa. Kuna wenye kampuni, wenye hisa nyingi, wale wenye hisa chache na wale hawana. Kura huwa na maana sana. Hamwezi kupiga kelele huko na kusema Rais William Ruto ni mbaya, halafu akipata na kuanza kugawa mnapanga foleni ili kupewa. Eti mnataka kuwapita wale walisema anafaa ili muwe hapo mbele. Inawezekana kweli? Katika Ikulu, kazi yangu ni kupanga hiyo foleni. Nikiona wewe ulipanda, nakutoa nyuma na kukupeleka mbele. Nikiona hukupanda, nakutoa mbele na kukupeleka nyuma,” akasema Bw Gachagua alipohutubu katika Kaunti ya Kericho Jumapili.

Matamshi hayo yameonekana kuwapa tumbojoto wanasiasa ambao wamekuwa wakihama kutoka Azimio na kujiunga na Kenya Kwanza wakilenga kuteuliwa kwenye nyadhifa tofauti serikalini.

Kufikia sasa, baadhi ya wanasiasa wa Jubilee ambao wameasi Azimio na kujiunga na Kenya Kwanza ni wabunge Sabina Chege (Mbunge Maalum), Kanini Kega (EALA), Samuel Arama (Nakuru Town West), Adan Keynan (Eldas), Rachael Nyamai (Kitui) kati ya wengine.

Katika chama cha ODM, wabunge tisa wamejitokeza na kutangaza kuanza kumuunga mkono Rais Ruto ili “kuyawezesha maeneo yao kupata maendeleo”.

Wabunge hao pia wamebuni vuguvugu maalum la “kulikomboa eneo la Nyanza” kutoka kwa ushawishi wa kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga.

Wabunge hao ni Gideon Ochanda (Bondo), Elisha Odhiambo (Gem), Mark Nyamita (Uriri), Caroli Omondi (Suba Kusini), Shakeel Shabir (Kisumu Mashariki), Felix Odiwuor maarufu ‘Jalang’o’ (Lang’ata), Paul Abuor (Rongo), John Owino (Awendo) na Seneta Tom Ojienda (Kisumu).

CAS

Ikizingatiwa kuwa mahakama juzi ilimruhusu Rais Ruto kuwateua Manaibu wa Mawaziri (CASs), wadadisi wanasema kuwa matamshi ya Bw Gachagua yanaonekana kuwalenga wanasiasa wa Azimio wanaomezea mate nyadhifa hizo.

“Kauli ya Bw Gachagua inawalenga wanasiasa ambao tayari wamehamia Kenya Kwanza kutoka Azimio kufahamu kuwa si lazima wapate nyadhifa wanazomezea mate,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Japo Rais Ruto “amerudishia mkono” baadhi ya washirika wake waliomuunga kwenye uchaguzi mkuu uliopita kwa kuwateua katika nyadhifa mbalimbali, wengi wao bado wako kwenye baridi.

Baadhi yao ni aliyekuwa Seneta wa Kakamega Cleophas Malala, wabunge wa zamani Caleb Kositany (Soy), Purity Ngirichi (Kirinyaga), Charles Njagua ‘Jaguar’ (Starehe), Benjamin Washiali (Mumias Mashariki), Cate Waruguru (Mbunge wa Kike wa Laikipia) kati ya wengine.

Baadhi ya wanasiasa wa Azimio waliohamia Kenya Kwanza na kufanikiwa kupata teuzi tofauti serikalini ni aliyekuwa gavana wa Kisumu, Jack Ranguma, wabunge wa zamani Omondi Anyanga (Nyatike) na George Oner (Rangwe).

Bw Ranguma, aliyewania ugavana wa Kisumu kwa chama cha MDG na kushindwa na Prof Anyang’ Nyong’o, aliteuliwa mwenyekiti wa Mamlaka ya Kusimamia Vyama vya Akiba na Mikopo (Sasra).

Naye Bw Anyanga aliteuliwa mwenyekiti wa Bodi ya Kawi ya Kinyuklia (KNRA) huku Bw Oner akitunukiwa wadhifa wa mwenyekiti wa Jopo kazi la Kuendesha Ujenzi wa Nyumba za Jamii ya Wanubi.

Hata hivyo, matamshi ya Bw Gachagua yamekosolewa vikali, akiambiwa kukoma kuigawanya nchi.

Wanasiasa ambao wamejitokeza kumkosoa ni Seneta Ledama Ole Kina (Narok), Seneta Dan Maanzo (Makueni), mbunge Junet Mohamed (Suna Mashariki), aliyekuwa mbunge wa Mukurwe-ini Kabando wa Kabando kati ya wengine.

“Ni sikitiko kuu kwa Bw Gachagua kuifananisha serikali na kampuni!” akasema Bw Kina.

Bw Maanzo alisema kuwa Bw Gachagua anafaa kuwa mwangalifu na matamshi anayotoa.

“Naibu Rais ni rafiki yangu kwani tulihudumu katika Bunge la Kitaifa. Hata hivyo, lazima awe mwangalifu ili kutoigawanya nchi,” akasema Bw Maanzo.

  • Tags

You can share this post!

Mwanasiasa ahofia mali yake kupigwa mnada

Ushawishi wa Uhuru wadidimia marafiki wakizidi kumtoroka

T L