• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 12:52 PM
Ushawishi wa Uhuru wadidimia marafiki wakizidi kumtoroka

Ushawishi wa Uhuru wadidimia marafiki wakizidi kumtoroka

NA MWANGI MUIRURI

WANDANI wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta wanamtoroka kwa wingi ishara kwamba kudidimia kwa ushawishi wa kisiasa wa kiongozi huyo wa chama cha Jubilee; ingawa ametangaza kuwa ataendelea kushiriki siasa.

Baada ya wabunge 30 kutoka chama hicho kukutana na Rais William Ruto na kutangaza mpango wa kujitenga na muungano wa upinzani, Azimio, wabunge hao wameendelea kumkosoa Bw Kenyatta.

Kwa mfano, Mbunge Maalum Sabina Chege ndiye wa hivi punde kumtaka Bw Kenyatta kutoa mwelekeo kwa chama hicho, haswa kutokana na mgawanyiko ulioko katika muungano huo wa upinzani.

Akiongea Jumapili, Mbunge huyo Mwakilishi wa zamani wa Murang’a pia anamtaka Bw Kenyatta kutoa mwelekeo kwa wanachama wa Jubilee kuhusina na mikutano ya kupinga serikali inayoendeshwa na Bw Raila Odinga kote nchini.

“Tulipokuwa tukimsubiri atoe mwelekeo, tulimwona akiwa juu ya lori jijini Kisumu (baada ya kuhudhuria mazishi ya waziri wa zamani wa elimu George Magoha) akitangaza kuwa kiongozi wa chama chake ni kiongozi wa ODM Raila Odinga,” Bi Chege akasema katika runinga ya Inooro TV.

Alishangaa ikiwa chama cha Jubilee kimemezwa na ODM.

Bi Chege ambaye aliongoza kampeni za urais za Odinga katika eneo la Mlima Kenya, alimkumbusha Bw Kenyatta kwamba “wandani wengi walipoteza katika uchaguzi sio eti walikwa wabaya bali ni kwa sababu waliamua kusimama nawe.”

“Binafsi nilikuwa nimeombwa na Kenya Kwanza niwe mgombea mwenza katika kinyang’anyiro cha ugavana Nairobi lakini nilikataa ombi hilo kwa sababu yake,” Bi Chege akadai, akirejelea uwezekano wake kuwa mgombea mwenza wa Bw Johnson Sakaja ambaye hatimaye aliibuka mshindi.

Matukio haya ya hivi punde yataweka kwa mizani weledi wa kisiasa wa Bw Kenyatta, haswa baada ya kuondoka mamlakani.

Lakini kwa miaka 26 iliyopita ameonekana kama mtu ambaye amekuwa akicheza mchezo wa pata potea katika ulingo wa siasa.

Lakini mkondo ambao ameamua kufuatia siku chache baada ya kustaafu ni ule ambao watangulizi wake wawili hawakuwahi kufuata.

Daniel Moi na Mwai Kibaki waliamua kujiondoa kutoka ulingo wa siasa baada ya kuwapokeza mamlaka warithi wao.

Hii ni licha ya kwamba mara kadha marehemu Moi alipenda kupokea jumbe za wanasiasa waliomtembelea nyumbani kwake Kabaraka, Nakuru kushauriana naye kuhusu masuala mbalimbali yenye “umuhimu wa kitaifa.”

Lakini kwa kuonyesha kuwa yu tayari kuendelea na siasa, hata baada ya kustaafu kama Rais, Bw Kenyatta anajiweka katika hatari ya kupokonywa malipo yake ya pensheni.

Wadadisi wa kisiasa wanasema huenda Rais huyo mstaafu anajiandaa kuendelea kutumia ushawishi wake, japo finyu, kusaidia wanasiasa fulani kushinda katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Lakini kwa sababu siasa ni mchezo wa bahati nasibu, huenda Bw Kenyatta akapoteza au akawashangaza mahasidi wake kwa kufaulu kwa kiwango katika mikakati yake ya kisiasa.

  • Tags

You can share this post!

Gachagua alipua vinyonga wa Azimio

Vijana Wapwani wasakwa kimataifa kuhusu ugaidi

T L