• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Gachagua, Karua waanika wazi ukwasi wao

Gachagua, Karua waanika wazi ukwasi wao

JUSTUS OCHIENG’ Na CHARLES WASONGA

MGOMBEA mwenza wa urais wa Kenya Kwanza Rigathi Gachagua na mwenzake wa Azimio Martha Karua Jumanne usiku walitangaza hadharani utajiri wao.

Bw Gachagua alifichua kuwa anamiliki mali ya thamani ya Sh800 milioni huku akipuuzilia madai kuwa Sh5 bilioni zilipitishwa katika akaunti zake za benki.

Kwa upande wake Bi Karua, alifichua kuwa anamiliki mali ya thamani ya Sh150 milioni.

Alieleza kuwa thamani ya mali yake ambayo ilikuwa Sh56 milioni mnamo 2013 ilipanda kutokana na mfumko wa bei za bidhaa.

“Nadhani thamani ya mali yangu ni Sh150 milioni na hii ni kwa sababu mali yangu ya thamani ya Sh56 milioni niliyotangaza 2013 imepanda kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha,” akasema.

“Sijawahi kupata mali nyingi. Sina uchu wa kumiliki ardhi. Usidhamini kuwa Martha Karua anatamani kuwa bilionea,” akasema wakati wa awamu ya pili ya mdahalo wa wagombea wenza wa urais katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki (CUEA), mtaani Karen, Nairobi.

Bw Gachagua alisema kuwa kesi za ufisadi zinazomwandama zimechochewa na serikali pamoja na Rais Uhuru Kenyatta na ndio maana zinajivuta mahakamani.

“Walituma maafisa wa usalama nyumbani kwangu na wakanikamata kama mwizi mwaka jana. Lakini tangu wakati huo, kesi hizo hazijaamuliwa kwa sababu hamna ushahidi wa kuzihimili,” akasema.

Bw Gachagua alimhusisha Bi Karua na sakata ya ufisadi ambapo inadaiwa alipokea hongo kutoka kampuni ya kutengeneza sigara ya British American Tobacco (BAT).

Aidha, mgombea mwenza huyo wa Naibu Rais Dkt William Ruto, alidai kuwa Bi Karua alitumia mamlaka ya afisi yake, akihudumu kama Waziri wa Haki, kunyakua ardhi katika eneo la South Ngariama na kuwagawia jamaa zake.

Bw Gachagua alisema chini ya utawala wa Kenya Kwanza taasisi husika zitapewa uhuru ya kuchunguza madai kama hayo ya ufisadi bila kuingiliwa na serikali kuu inavyofanyika sasa chini ya serikali ya Jubilee.

Lakini Bi Karua alikuwa mwepesi wa kujitetea dhidi ya madai ya Bw Gachagua akisema kuwa madai hayo hayana msingi wowote.

“Ningependa kumfahamisha Gachagua kuwa sina kipande cha ardhi popote nchini, isipokuwa ardhi ambako ninaishi Nairobi na kipande cha ardhi cha familia ambacho nilipewa na wazazi wangu Gichugu, Kirinyaga,” akaeleza.

“Ninatoa changamoto kwa serikali hii na serikali ya kaunti ya Kirinyaga kwamba ikiwa niko tayari kuchunguzwa na ikiwa kuna ukweli wowote nipelekwe kortini na mali hiyo itwaliwe,” Bi Karua akasema

Kuhusiana na sakata ya BAT, alisema pesa zinazodaiwa alipokea zilielekezwa katika sekritariati ya kampeni zake na mfadhili fulani.

“Pesa hizo hazikulipwa katika akaunti yangu. Baadaye ilibainika kuwa pesa hizo zilitoka kwa kampuni fulani. Suala hilo limechunguzwa na Uingereza na faili hiyo ikafungwa,” akajitetea Karua.

  • Tags

You can share this post!

Kalonzo atikisa Azimio na wito wa suti ya Wiper Kitui

Raha tele mwanariadha Kasyoka akimtunuku baiskeli daktari...

T L