• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 11:37 AM
Kalonzo atikisa Azimio na wito wa suti ya Wiper Kitui

Kalonzo atikisa Azimio na wito wa suti ya Wiper Kitui

NA BONIFACE MWANIKI

KINARA wa chama cha Wiper, Bw Stephen Kalonzo Musyoka, amerai wakazi wa eneo la Ukambani kumpa uwezo wa kutetea maslahi yao kwa kumchagulia viongozi wa chama chake cha Wiper pekee, kwenye uchaguzi mkuu Agosti 9.

Akizungumza katika maeneo ya Nguni na Mutha, Kaunti ya Kitui, alipowapigia debe wawaniaji wa Wiper, Bw Musyoka alisema kuwa kupigia muungano wa Azimio bila kumchagulia wawaniaji wa chama chake ni sawa na kumtuma vitani bila wanajeshi wa kumpigania.

“Nataka mnichagulie viongozi wa chama cha Wiper pekee, mkianzia na gavana wa kaunti ya Kitui, seneta, mwakilishi wa kina mama na pia wawakilishi bunge,” akasema.

Alieleza kukerwa na tabia ya viongozi kadhaa kutoka eneo hilo, ambao hutumia jina lake kujinufaisha kisiasa, lakini baadaye wanamsaliti na kupanga njama dhidi yake.

“Kuna wanasiasa wa eneo hili ambao wamekuwa wakitumia jina langu kupata umaarufu. Wakishapata nyadhifa wanaanza kunipiga vita. Sasa nataka hapa Kitui mnichagulie Bwana Malombe kama gavana wenu. Nataka mnipe viongozi wa Wiper ili nipate nguvu Kitaifa,” akasema.

Matamshi yake huenda yanatokana na pingamizi alizopata kutoka kwa magavana watatu wa sasa Ukambani; Charity Kaluki Ngilu (Kitui), Dkt Alfred Mutua (Machakos) na Prof Kivutha Kibwana (Makueni).

Hatua ya Bw Musyoka kufanya kampeni za kuwaunga mkono wawaniaji wa chama chake katika eneo la Ukambani, imezua tumbojoto miongoni mwa viongozi wengine katika muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya.

Aliyeathiriwa zaidi ni aliyekuwa seneta wa Kitui, Bw David Musila anayegombea Kiti cha ugavana wa kaunti ya Kitui kwa Chama cha Jubilee.

Bw Musila amejitokeza waziwazi kuwataka wakazi wa Kitui wawe na uhuru wa kujichagulia viongozi wanaotaka, bila ya kushurutishwa na yeyote.

“Si jambo zuri kwa kiongozi kama Kalonzo Musyoka kuwashurutisha wakazi wa Kitui wamchague yeyote. Sote tumo kwenye Muungano wa Azimio na ni vyema viongozi wote wapewe fursa ya kufanya kampeni na kuchaguliwa kulingana na uwezo walio nao. Ningependa kuwaonya wakazi wa Kitui wasikubali kulazimishwa kufanya maamuzi. Chagueni kiongozi kulingana na uwezo wake,” akalalama Bw Musila.

  • Tags

You can share this post!

Mwaniaji alenga kura kwa ahadi ya pombe

Gachagua, Karua waanika wazi ukwasi wao

T L