• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
Gachagua, Raila wakaa ngumu

Gachagua, Raila wakaa ngumu

JAMES MURIMI Na JUSTUS WANGA

NAIBU wa Rais Rigathi Gachagua na kinara wa Azimio Raila Odinga mnamo Alhamisi walishikilia misimamo yao mikali huku wakisema hawako tayari kwa mazungumzo baina ya serikali na Upinzani.

Bw Odinga alikanusha madai anaongoza maandamano ili ‘akiribishwe’ katika serikali ya Kenya Kwanza.

Akizungumza katika jumba la Capitol Hill, Nairobi, Bw Odinga alishikilia kuwa anachotafuta ni ukweli kuhusu uchaguzi wa Agosti 9, 2022.

“Wanasiasa wa Kenya Kwanza wamekuwa wakidai ninatafuta handisheki. Hayo ni madai yasiyo na mashiko na matusi kwa Wakenya,” akasema Bw Odinga.

“Hatuwezi kuungana na serikali haramu,” alisema Bw Odinga huku akiongezea kuwa: “Jibu letu kwa viongozi wa kidini kuhusu wito wa kutaka kuwepo mazungumzo ni Injili ya Yohana 8:32.”

Bw Gachagua kwa upande mwingine pia alipuuzilia mbali wito wa kuwepo kwa mazungumzo kati ya Rais William Ruto na Bw Odinga ili kumaliza maandamano.

“Nyinyi viongozi wa kidini tumewasikia na tunawaheshimu. Lakini kwa nini mnatutaka kufanya mazungumzo na mtu ambaye amekuwa akituhujumu?” akauliza Bw Gachagua.

Bw Odinga ametangaza maandamano mara mbili kwa wiki – Jumatatu na Alhamisi – kushinikiza serikali kupunguza bei ya bidhaa, kurejesha ruzuku ya mafuta, kusitisha mchakato wa kuteua makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi wa Mipaka (IEBC), kukomesha ukabila katika idara za serikali na kufungua hifadhi ya matokeo ya urais ya uchaguzi wa Agosti 9, 2022.

Bw Odinga pia anataka serikali kutimua manaibu wa mawaziri (CAS) 50 walioapishwa Alhamisi.

  • Tags

You can share this post!

Mwanahabari mkongwe apumzishwa

Hofu hatua za Rais zanyonga demokrasia

T L