• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Gesami akanusha madai alitaka Gavana Nyaribo amwage unga

Gesami akanusha madai alitaka Gavana Nyaribo amwage unga

NA WYCLIFFE NYABERI 

NAIBU Gavana wa Kaunti ya Nyamira Dkt James Gesami amekanusha madai kwamba alihusika katika njama ya upangaji wa hoja iliyolenga kumng’atua mamlakani Gavana Amos Nyaribo.

Hoja hiyo iliwasilishwa katika Bunge la Kaunti ya Nyamira na diwani wa Esise Josiah Mang’era wiki jana lakini ilianguka baada ya kukosa kufikisha kigezo cha thuluthi mbili jinsi inavyotakikana kisheria.

Baada ya kunusurika kutimuliwa, gavana Nyaribo aliwaambia wanahabari mnamo Jumatano kwamba alikuwa na ushahidi kwamba naibu wake alishurutisha baadhi ya madiwani wamng’atue, jambo ambalo Dkt Gesami amelikana.

Baada ya kupata afueni hiyo, gavana Nyaribo aliuliza alikokuwa Gesami akidai aliwahonga baadhi ya madiwani akiwataka wapige kura ya kumwondoa ofisini.

“Alikuwa wapi? Muulize alikokuwa wakati kulikuwa na vita. Tunazo sauti akizungumza na baadhi ya madiwani akiwaambia waning’atue na mkitaka tutawapatia,” Nyaribo alidai lakini hakupeana sauti hizo alizosema ni za kurekodiwa.

Siku moja baadaye, kwenye taarifa kwa wanahabari, mbunge huyo wa zamani wa Mugirango Magharibi alisema hakuhusika kwa vyovyote katika upangaji wa hoja hiyo iliyotibuka.

“Ningependa kujitenga na madai kwamba niliwalipa baadhi ya madiwani wamng’atue Nyaribo. Vile vile ninapuuzilia mbali madai kuwa mke wangu naye alifanya hivyo. Ikiwa kuna ushahidi ambao mtu yeyote anao, basi aulete,” Gesami akasema.

Nyaribo na Gesami hawajakuwa na mlahaka mzuri wa kikazi. Viongozi hao wawili walitofautiana muda mfupi tu baada ya kushinda ugavana wa Nyamira.

Mzozo kati yao ulianza pale gavana Nyaribo alipoteua Baraza la Mawaziri. Dkt Gesami alisema hakupewa dili nzuri katika teuzi hizo jinsi walivyoahidiana kabla ya uchaguzi.

Tangu siku hiyo, ni nadra kuwaona viongozi hao wakionekana pamoja kwenye hafla za umma.

Nyaribo aliponea hoja ya kubanduliwa kwake baada ya madiwani 18 kupinga hoja ya kumwondoa. Ni madiwani 16 waliotaka ‘kumsulubisha’.

Kiongozi huyo wa chama cha United Progressive Alliance (UPA) amesema sasa hoja hiyo ni jambo lililopitwa na wakati na amewataka madiwani kushirikiana naye kuwahudumia wakazi wa Nyamira.

  • Tags

You can share this post!

Maina Njenga: Gachagua akitaka ‘patanisho’ na...

Rising Starlets kukaribisha Angola uwanjani Nyayo

T L