• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Maina Njenga: Gachagua akitaka ‘patanisho’ na Uhuru alete mbuzi wa matambiko

Maina Njenga: Gachagua akitaka ‘patanisho’ na Uhuru alete mbuzi wa matambiko

NA MWANGI MUIRURI

ALIYEKUWA kiongozi wa kundi haramu la Mungiki Bw Maina Njenga amesema Jumamosi akiwa Murang’a kwamba Wakenya wanalipa ushuru wa juu kwa sababu “sisi ndani ya Azimio La Umoja-One Kenya tuliwaambia mkatupuuza”.

Wakenya wengi wanalia kuwa gharama ya maisha imepanda kwa sababu serikali ya Kenya Kwanza ikiongozwa na Rais William Ruto inawatoza ushuru wa juu mno.

Na wakati huo huo, Bw Njenga amewataka wafuasi wake kurudisha kondoo walioiba kutoka kwa shamba la familia ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta la Northlands.

“Baadhi ya vijana wanaonishabikia kisiasa waliiba kondoo Northlands na ninawaagiza wawarudishe huko,” akasema Bw Njenga.

Akionekana kuzungumza kwa niaba ya vijana wa eneo la Mlima Kenya, kiongozi huyo wa zamani wa Mungiki amemtaka Naibu Rais Rigathi Gachagua aache kuwaandama wapiganiaji wa masilahi ya vijana Mlima Kenya na kuwaona kama maadui.

Amefichua kuwa yuko tayari kumpatanisha Bw Gachagua na Bw Kenyatta bora tu “Gachagua awe tayari kuleta mbuzi wa matambiko”.

Pia amemtaka Rais Ruto afahamu kwamba vijana wa eneo la Mlima Kenya si wapenda utengano na kwamba mambo yao matatu yenye umuhimu mkubwa ni umoja, upendo na ufanisi.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mwenyekiti wa Kongamano la Wanaume wa Agikuyu Bw Thuo Mathenge almaarufu ‘Wanguku’ amesema Bw Gachagua angejumuika nao lakini ameenda Meru kwa hafla nyingine yenye umuhimu wa kitaifa.

“Hivu karibuni mtaona Bw Gachagua, Bw Kenyatta na Bw Njenga wakijumuika kwenye jukwaa moja kwa lengo la kuunganisha wenyeji na wakazi wa Mlima Kenya,” akasema Bw Wanguku.

  • Tags

You can share this post!

Wapangaji wajionea sinema ya bure landilodi akidaiwa na...

Gesami akanusha madai alitaka Gavana Nyaribo amwage unga

T L