• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Hakuna deni katika siasa, Atwoli awaambia wanaolenga Ikulu 2022

Hakuna deni katika siasa, Atwoli awaambia wanaolenga Ikulu 2022

Na LEONARD OMYANGO

KATIBU Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU), Bw Francis Atwoli amewataka wanasiasa wanaotaka ‘kurudishiwa mkono’ mwaka 2022 wasahau hilo huku akisema kuwa hakuna deni katika siasa.

Bw Atwoli aliyekuwa akizungumza Jumapili wakati wa hafla ya maombi kwa ajili ya Siku ya Wafanyakazi itakayoadhimishwa Jumanne katika Kanisa Katoliki la St Stephens Cathedral, Barabara ya Jogoo, Nairobi, alisema wanasiasa wanaongoja kurudishiwa mkono wataambulia patupu 2022 wasipojipanga wenyewe mapema.

Bw Atwoli alionekana kumrejelea Naibu wa Rais William Ruto pamoja na vinara wenza wa NASA Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC) na Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) ambao wamekuwa waakitarajiwa kurudishiwa mkono mwaka 2022.

Bw Ruto anatarajia kuungwa mkono na Rais Kenyatta kwa kumsaidia kushinda uchaguzi wa 2013 na 2017.

Nao vinara wa NASA Bw Musyoka, Bw Mudavadi na Seneta wa Bungoma Wetang’ula wamekuwa wakimshinikiza kiongozi wa ODM Raila Odinga kuwalipa deni la kisiasa kwa kumuunga mkono katika uchaguzi mkuu uliopita.

“Katika siasa hakuna deni. Siku moja katika siasa ni sawa na miaka 100, kwa hivyo wanaongojea kulipwa madeni ya kisiasa wasahau,” akasema Bw Atwoli.

Huku kiongozi huyo wa wafanyakazi akisema hayo, Kiongozi wa Wengi Bungeni, Bw Aden Duale alisema kuwa urais wa Kenya si ufalme ambao hurithiwa na watu kutoka familia fulani tu.

 

Duale ampigia debe Ruto

Bw Duale aliyekuwa akizungumza katika eneo la Garissa, alisema Wakenya watachagua Bw Ruto 2022 kutokana na rekodi ya maendeleo iliyofanywa na serikali ya Jubilee.

“Bw Ruto alikuwa mkulima, wengine ni watoto wa matajiri. Wakenya watachagua mchapa kazi wala si mtoto wa matajiri,” akasema Bw Duale.

Wakati huohuo, Bw Atwoli pia alisema wafanyakazi wa humu nchini wanaunga pendekezo lililotolewa na Bw Odinga la kutaka Katiba ibadilishwe ili kubuniwe serikali za ngazi tatu.

Alisema mfumo huo wa serikali za ngazi tatu utasaidia rasilimali kufikia Wakenya katika maeneo yote kwa usawa.

Wiki iliyopita, Bw Odinga alihimiza kubuniwa kwa serikali ya ngazi tatu; serikali ya kitaifa, serikali 14 za kanda na kaunti 47 huku akisema mfumo huo utahakikisha kuwa kuna usambazaji sawa wa rasilimali.

Pendekezo hilo, hata hivyo limepingwa vikali na Naibu wa Rais, Bw Ruto, Bw Mudavadi, Seneta Wetang’ula na aliyekuwa Seneta wa Kakamega Boni Khalwale.

Viongozi hao wanasema kuwa kubuniwa kwa serikali 14 za kanda kutatatiza utendakazi wa serikali za kaunti.

 

Usiwe kizuizi

“Sisi wafanyakazi tunaunga kubuniwa kwa serikali za kanda. Ikiwa Rais Kenyatta na Bw Odinga wameafikiana kuwa wanataka kubadili Katiba, wewe ukiwa kizuizi njiani basi utasombwa na mawimbi,” akasema Bw Atwoli.

“Juzi nimesikia Bw Khalwale akisema kuwa ataongoza wanaopinga kubadilishwa kwa rasmu ya Katiba. Ikiwa yeye alishindwa kura za ugavana katika Kaunti ya Kakamega, atapata wapi kura za kuzuia Katiba kupitishwa?” akaongezea.

Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja, Mwakilishi wa Kike wa Nairobi Esther Passaris, wabunge Wilson Sossion (Maalum) na George Aladwa walisema kuwa wanaunga mkono pendekezo la kutaka Katiba ifanyiwe marekebisho.

“Ikiwa kubadilishwa kwa Katiba ndiko kutafanya Wakenya kuungana na kuzika ukabila katika kaburi la sahau basi tuko tayari kwa ajili ya mabadiliko hayo,” akasema Bw Sakaja.

You can share this post!

JAMVI: Wito wa kurekebisha Katiba wazua uhasama wa mbio za...

Mahangaiko ya mafuriko shule zikifunguliwa

adminleo