• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Hatua ya Ruto kunasa vyama vidogo hatari kwa upinzani

Hatua ya Ruto kunasa vyama vidogo hatari kwa upinzani

NA CECIL ODONGO

HATUA ya Rais Mteule William Ruto kuvutia upande wake wabunge wa kujitegemea na wale wa vyama vilivyo ndani ya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya inalenga kusambaratisha upinzani Bungeni.

Siku chache tu baada ya kutangazwa mshindi wa Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, Rais Mteule Dkt William Ruto ameanza mikakati ya kubomoa upinzani kwa kuwashawishi baadhi ya viongozi wa mrengo wa Azimio kuhamia Kenya Kwanza.

Mnamo Alhamisi, Dkt Ruto aliwapokea wabunge saba wa chama cha United Democratic Movement (UDM) kinachoongozwa na Gavana wa Mandera, Ali Roba ambaye alishinda kiti cha Useneta kwenye uchaguzi wa wiki jana.

Dkt Ruto tayari amenyakua wabunge 10 kati ya 12 waliochaguliwa kwa tiketi ya kujitegemea.

Miongoni mwa wabunge wateule wa kujitegemea ambao wametangaza uaminifu wao kwa Dkt Ruto ni Geoffrey Ekesa Mulanya (Nambale), Njoroge Kururia (Gatundu Kaskazini), Nebart Muriuki (Mbeere Kusini), Abdul Rahim Dawood (Imenti Kaskazini) na Monica Muthoni (Lamu).

Kulingana na duru ndani ya Kenya Kwanza, Dkt Ruto pia analenga kuvamia chama cha National Ordinary People’s Empowerment Union (Nopeu) ambacho kilishinda ubunge wa Tigania Mashariki kupitia kwa Bw Mpuru Aburi.

UDM na Nopeu ni miongoni mwa vyama 26 vilivyo katika muungano wa Azimio.

Jana Ijumaa, kinara wa Azimio la Umoja, Raila Odinga alishutumu vikali Dkt Ruto kwa kujaribu kulemaza Azimio huku akisema hatua hiyo inalenga kurejesha nchi katika ‘enzi ya udikteta ya Kanu ambapo wanasiasa wa upinzani walihongwa kuunga mkono serikali’.

Bw Odinga alisema kuwa wabunge wa UDM wangali chini ya Azimio kwa kuwa hawajajiondoa kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na mkataba wa Azimio.

“Ruto asirejeshe nchi katika enzi za Kanu kwa kuhonga wabunge wa vyama pinzani. Tunawasihi wabunge wa Azimio na wale wa kujitegemea kuwa imara – wasikubali kuhongwa na kuingia Kenya Kwanza,” akasema Bw Odinga kupitia kwa msemaji wake Prof Makau Mutua.

Kwa sasa, muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Rais Mteule Ruto, una wabunge 159 huku Azimio ikiongoza kwa wabunge 161.

Baada ya kuvutia upande wake wabunge wa kujitegemea na wale wa vyama vya Azimio, Kenya Kwanza sasa inaungwa mkono na wabunge wasiopungua 176.

Jana Ijumaa, Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni alionya wabunge wateule 26 wa chama hicho dhidi ya kujiunga na Kenya Kwanza huku akisema kuwa watapoteza viti vyao.

Bw Kioni alitoa onyo hilo siku moja baada ya Naibu Rais Mteule Rigathi Gachagua Alhamisi kudokeza kwamba, wabunge wa Jubilee watahamia Kenya Kwanza baada ya Dkt Ruto kuapishwa kuwa Rais wa Tano wa Kenya.

Iwapo Dkt Ruto atafanikiwa kuvutia upande wake wabunge 233 – yaani theluthi mbili ya wabunge – atakuwa ameafikia idadi inayohitajika kufanya maamuzi makubwa ikiwemo kufanyia mabadiliko baadhi ya vifungu vya Katiba.

Kwa kudhibiti Bunge la Kitaifa na kulemaza kabisa upinzani, Dkt Ruto atapitisha ajenda za serikali yake Bungeni bila pingamizi na Bunge litapoteza uwezo wa kutathmini utendakazi wa serikali.

Wadadisi wanasema kuwa, Dkt Ruto sasa anasaka idadi kubwa ya wabunge kumwezesha kupata nyadhifa za uspika katika Bunge la Kitaifa na Seneti.

Dkt Ruto anataka kujivunia wabunge wengi ili iwapo ushindi wake utafutwa na Mahakama ya Juu, basi atakuwa na idadi ya kutosha ya wabunge kumsaidia kufanya kampeni kutetea ushindi wake.

Mnamo 2014, Jubilee wakati huo chini ya uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta na Dkt Ruto ilitumia idadi yao kubwa Bungeni kupitisha Mswada wa Kurekebisha Sheria za Usalama kwenye kikao kilichogubikwa na ghasia bungeni.

Vifungu kadhaa vya sheria hiyo vilitupwa na korti baada ya kubaini kuwa vilikiuka Katiba kwa kukandamiza uhuru wa kuzungumza.

Wadadisi wanasema Dkt Ruto akiungwa mkono na idadi kubwa ya wabunge anaweza kutumia mwanya huo kutimua naibu wake Rigathi Gachagua iwapo watakosana kabla ya kukamilisha muhula wao wa kwanza 2027 na kukandamiza taasisi huru kama vile Idara ya Mahakama.

Bw Martin Andati, mdadisi wa masuala ya kisiasa, hata hivyo, anasema Dkt Ruto huenda akashindwa kudhibiti idadi kubwa ya wabunge kwa muda mrefu.

Profesa Macharia Munene, mhadhiri wa Sayansi ya Siasa, anasema kuwa itakuwa vigumu kwa Dkt Ruto kuungwa mkono na wabunge 233.

  • Tags

You can share this post!

Mashirika ya kijamii yasema uchaguzi wa Agosti 9 ulisheheni...

Wazazi wataka Wizara ya Elimu iongeze muda wa masomo katika...

T L