• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Hila ya Uhuru kuwa na nguvu akistaafu

Hila ya Uhuru kuwa na nguvu akistaafu

NA MWANGI MUIRURI

RAIS Uhuru Kenyatta analenga kutumia wabunge wa Jubilee kudhibiti serikali ya kinara wa ODM Raila Odinga iwapo atachaguliwa kuwa rais Agosti 9.

Rais Kenyatta pia analenga kutumia cheo cha naibu wa rais na mawaziri atakaotengewa kudhibiti serikali ya Bw Odinga.

Taifa Leo imefahamishwa kuwa viongozi wa Jubilee wanataka chama cha ODM kutosimamisha wawaniaji wa ubunge katika ngome zake hasa Mlima Kenya, Nairobi na baadhi ya sehemu za Rift Valley, na pia za vyama washirika wake, ili kukiwezesha kuwa na idadi kubwa ya wabunge.

Ikiwa Jubilee na vyama vidogo washirika wake watakuwa na wabunge wengi, Rais Kenyatta kama kiongozi wake atakuwa na ushawishi mkubwa ndani ya serikali ya Bw Odinga.

Mwezi Februari Jubilee kilimwidhinisha Rais Kenyatta kuendelea kuwa kiongozi wake kwa miaka mitano. Hii inampa mamlaka ya kuwapa maagizo wabunge wa chama hicho na washirika wao katika mabunge ya Taifa na Seneti kuhusu mwelekeo anaotaka wachukue.

Katika juhudi za kuhakikisha Jubilee kitakuwa na wabunge wengi na maseneta, chama hicho kimeshawishi vyama vidogo kujiunga na mrengo wa Azimio kupitia kwake. Vyama hivyo ni pamoja na PAA chake Gavana Amason Kingi wa Kilifi (Pwani), DAP-K cha Eugene Wamalwa (Magharibi), PNU cha Waziri wa Kilimo Peter Munya (Mlima Kenya Mashariki) na UPYA cha Waziri wa Fedha Ukur Yatani (Kaskazini Mashariki).

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka (Ukambani) pia anatarajiwa kujiunga na Azimio kupitia Jubilee. Mnamo Februari 26, alieleza kuwa uamuzi wao kujiunga na Azimio ni kutokana na imani yao kwa Rais Kenyatta na wiki iliyopita alionyesha kutomwamini Bw Odinga akisema hana uaminifu wa kutimiza ahadi.

Iwapo mikakati hii itafanikiwa, Rais Kenyatta anatarajia kuvuna wabunge wengi isipokuwa Nyanza ambayo ni ngome ya Bw Odinga na Rift Valley kwake Naibu Rais William Ruto.

USEMI MKUBWA

Katibu Mkuu mpya wa Jubilee, Jeremiah Kioni aliambia Taifa Leo kuwa Rais Kenyatta amejitolea kuhakikisha kuwa atakuwa na usemi mkubwa katika Bunge la Kitaifa na Seneti.

“Kinyang’anyiro cha urais ni baina ya Ruto na Raila, na wote wanatoka nje ya eneo la Mlima Kenya. Bila kuwa na ushawishi Bungeni na Seneti masilahi yetu yatapuuzwa,” akasema Bw Kioni.

“Bajeti na sheria hupitishwa katika bunge, hivyo basi ni lazima tujipange tunyakue viti vingi iwezekanavyo ili tuwe na usemi wa kushawishi sera za kiserikali kutufaa,” akaongeza.

Kulingana na Mbunge wa Cherangany, Joshua Kutuny, Rais Kenyatta ataendelea kucheza siasa hata akistaafu: “Kuna tofauti kati ya kustaafu katika ofisi na siasa. Uhuru atakuwa mshauri wa Bw Odinga akiwa rais.”

Aliyekuwa Mbunge wa Gatanga, Peter Kenneth alisema wanajizatiti kuhakikisha mrengo wa Rais Kenyatta utakuwa na ushawishi mkubwa katika serikali ijayo.

BARAZA LA MAWAZIRI

Mkakati mwingine ambao Rais Kenyatta anatarajiwa kutumia kumdhibiti Bw Odinga ni kusukuma makubaliano na ODM kuhusu ugawaji wa nyadhifa katika Baraza la Mawaziri na vyeo vingine vya juu serikalini.

Baadhi ya mawaziri wa sasa wanatarajiwa kuwa kwenye baraza la Bw Odinga iwapo atashinda urais. Hawa ni pamoja na Mutahi Kagwe (Afya), Najib Balala (Utalii), Wamalwa (Ulinzi), Munya (Kilimo) na Yatani, ambao licha ya kuwa wanasiasa walikosa kujiuzulu kuwania vyeo vya kisiasa kwa kile kinaaminika ni ahadi ya kuteuliwa tena Azimio ikishinda.

Rais Kenyatta pia anatarajiwa kuwa na ushawishi katika utawala wa Bw Odinga kupitia kwa cheo cha naibu rais, ambacho Jubilee inasisitiza sharti mkaliaji wake ateuliwe kutoka Mlima Kenya. Kwa sasa wanaopigiwa upatu kuteuliwa ni Kenneth, Munya, Kagwe na Kiongozi wa Narc Kenya, Martha Karua.

Kwa upande mwingine, mrengo wa Kenya Kwanza wake Naibu Rais William Ruto umelalamika kuwa rais anasukumiza Bw Odinga awe rais ili yeye aendelee kuongoza kupitia kwa ‘rais kinyago’.

  • Tags

You can share this post!

Washukiwa 16 wakamatwa kuhusiana na kisa cha kudhulumiwa...

Pigo kwa Man-City beki tegemeo Ruben Dias akitarajiwa...

T L