• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
Hisia mseto serikalini baada ya Ukur Yattani kujaza nafasi ya Rotich

Hisia mseto serikalini baada ya Ukur Yattani kujaza nafasi ya Rotich

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE na maseneta wametoa hisia mseto kuhusu uteuzi wa Waziri wa Leba Ukur Yatani kuwa kaimu Waziri wa Fedha Jumatano alasiri.

Miongoni mwa maseneta wanne waliosema na Taifa Leo Dijitali katika majengo ya bunge saa chache baada ya tangazo hilo kutolewa ni Seneta wa Nandi Samson Cherargei aliyepinga uteuzi huo uliofanywa na Rais Uhuru Kenyatta katika mabadiliko machache aliyefanya katika serikali yake.

Bw Cherargei ambaye ni mwandani wa karibu wa Naibu Rais William Ruto alikejeli uteuzi wa Bw Yattani akimtaja kama “mtetezi wa vuguvugu la The Embrace“.

“Yattani hawezi kuleta mabadiliko yoyote katika Hazina ya Kitaifa kwa manufaa ya taifa kwa sababu tayari ameonyesha kuwa anaegemea mrengo fulani wa kisiasa. Juzi tulimwona akiwalaki wanachama wa kundi la Embrace katika kaunti ya Marsabit ilhali tunajua kuwa kundi hilo ni kipaza sauti cha mrengo fulani wa kisiasa,” akasema.

Kundi la “Embrace” linawaleta pamoja viongozi wanawake wanaopigia debe muafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga. Baadhi ya wanachama wake ni Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru, Waziri Msaidizi wa Wizara ya Vijana Rachel Shebesh na wabunge Gladys Wanga (Homa Bay), Gathoni wa Muchomba (Kiambu), Rosa Buyu (Kisumu) miongoni mwa wengine.

Hata hivyo, maseneta Johnston Sakaja (Nairobi), Kimani Wa Matangi (Kiambu) na George Khaniri (Vihiga) waliunga mkono uteuzi wa Bw Yattani ambaye alihudumu kama Gavana wa Marsabit kati ya 2013 hadi 2017.

“Naunga mkono hatua hii ambayo Rais alichukua Jumatano. Naamini kuwa kwa sababu Bw Yattani alikuwa Gavana wa Marsabit mojawapo ya kaunti zilizasalia nyuma kimaendeleo, atapiga jeki ugatuzi. Nataka afanye hivyo kwa kutanzua mzozo ulioko sasa kuhusu ugavi wa mapato,” akasema Bw Sakaja.

Bw Wa Matangi alitoa kauli sawa na hiyo akimtaka Bw Yattani kuhakikisha kuwa serikali ya kaunti zinatengewa fedha za kutosha katika mwaka huu wa kifedha.

“Kwa nampongeza Rais kwa kujaza nafasi hiyo haraka baada ya Bw Henry Rotich kushtakiwa kuhusiana na sakata ya ufisadi. Kwa sababu anaeleza mahitaji ya serikali za kaunti na serikali ya kitaifa natumaini kuwa atasaidia kusuluhisha mvutano wa sasa kuhusu ugavi wa mapato,” akaongeza Bw Wa Matangi.

Naye Bw Khaniri alimtaka Bw Yattani kuanza kazi haraka iwezekanavyo ikizingatiwa kuwa Wizara ya Fedha ni yenye umuhimu mkubwa kwa taifa.

“Vile vile, namtaka Bw Yattani kuhakikisha kuwa anashirikiana na Seneti na Bunge la Kitaifa katika shughuli zinazohusu utendakazi wa asasi hizo. Lakini kwa sababu amekuwa gavana wa Marsabit naamini atasukuma ajenda ya ugatuzi kuliko alivyofanya Bw Rotich,” akaeleza Bw Khaniri.

Uteuzi wa Yattani unajiri siku moja baada ya Bw Rotich na maafisa wengine 28 wa serikali kufunguliwa mashtaka kuhusiana na sakata ya ufisadi katika mradi wa ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer katika kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Na wakati huo huo, wabunge Chachu Ganya (Horr Kaskazini), Dido Rasso (Saku), Peter Kaluma (Homa Bay Mjini), Jared Okello (Nyando) na Alfredf Keter (Nandi Hills) walichangamkia uteuzi wa Bw Yattani wakisema anahitimu kwa kazi hiyo.

“Huyo ni mtu ambaye amehudumu katika utumishi wa umma kuanzia ngazi ya Mkuu wa Tarafa hadi Waziri. Naamini kuwa atatekeleza wajibu aliopewa kwa uelewa mkubwa,” akasema Bw Okello.

Nao Mbw Rasso na Ganya walimpongeza Rais Kenyatta kwa kumteua mtu kutoka jamii ndogo na eneo la Kaskazini mwa Kenya kwa wadhifa huo muhimu.

“Rais ameonyesha wazi kuwa anajali watu kutoka maeneo ambayo yaliachwa nyuma kimaendeleo tangu taifa hili lipate uhuru. Natumai kuwa uteuzi huu utafungua milango ya mambo mengine mazuri katika eneo letu,” akasema Bw Rasso.

  • Tags

You can share this post!

Kenya yarejeshea TZ dhahabu ya Sh100m

Wakenya hutumia WhatsApp, Facebook sana usiku –...

adminleo