• Nairobi
  • Last Updated April 12th, 2024 4:55 PM
Hiyo Nadco Azimio tulitoka bure, asema Karua

Hiyo Nadco Azimio tulitoka bure, asema Karua

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Narc-Kenya Martha Karua amesema kuwa muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya ulitoka mikono mitupu katika mazungumzo kati yake na mrengo wa Kenya Kwanza (KKA).

Kwenye mahojiano na runinga ya Citizen mnamo Alhamisi usiku, Bi Karua alidai wanachama wa Azimio katika Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (Nadco) walisaidia KKA kuendeleza ajenda zao.

“Kwa mtazamo wangu, mazungumzo hayo hayakuzaa matunda yoyote kwa sababu hakuna muafaka uliofikiwa kuhusu ajenda zetu tatu kuu ambazo ni gharama ya maisha, haki katika uchaguzi, na heshima kwa demokrasia ya vyama vingi,” akasema Bi Karua.

Akaongeza: “Muafaka ulipatikana kuhusu ajenda za Kenya Kwanza kama vile kuundwa kwa afisi ya kiongozi rasmi wa upinzani, na kuhalalishwa kwa afisi ya Mkuu wa Mawaziri, ambazo tayari Ruto alikwisha kuwasilisha bungeni.”

Kiongozi huyo wa Narc Kenya alieleza kuwa vikao vya kamati ya Nadco vilivyodumu kwa miezi minane vilikuwa ni vya kuwapotezea Wakenya hela na muda kwa sababu serikali haikuongozwa na nia njema iliposhiriki mazungumzo na upinzani.

“Mazungumzo hayo yalilenga kutuchezea shere na kutuliza maandamano. Matokeo ya mazungumzo yetu na utawala wa KKA hayakuzaa matunda yoyote kwa sababu Wakenya bado wanaumizwa na kupanda kwa gharama ya maisha. Kwa mtazamo wangu, ripoti ya Nadco haina maana yoyote kwa Wakenya kwa sababu haishughulikii madhila yao,” Bi Karua, ambaye alikuwa ni mgombea mwenza wa Raila Odinga katika uchaguzi wa urais wa Agosti 9, 2022, akaongeza.

Alielekeza lawama kwa utawala wa Kenya Kwanza kwa kile alichodai ni kufeli kufikiwa kwa malengo ya mazungumzo yake na upinzani.

“Licha ya sisi kama upinzani na wananchi kuendelea kuushinikiza utawala huu upunguze gharama ya maisha, walipuuza na badala yake kuendelea kuongeza bei ya bidhaa za kimsingi na kuanzisha aina nyingine za ushuru,” akasema.

Ili mazungumzo yoyote yafaulu, kulingana na Bi Karua, chama au mrengo ulioko mamlakani ni sharti kuonyesha nia njema kwa sababu wao ndio wanasukumwa kutimiza matakwa ya wananchi.

Kiongozi huyo wa Narc-Kenya aliutaja utawala wa sasa kama ambao hauheshimu sheria na maamuzi ya mahakama.

“Utawala huu unaendesha majukumu ya serikali kwa namna ambayo haijeshimu sheria na kudharau maoni ya wananchi ulivyofanya wakati wa ukusanyaji maoni ya umma kuhusu Sheria ya Fedha,” akasema.

“Unapodharua Katiba na watu ambao walikupa mamlaka na matakwa ya wengi, unageuka serikali mbaya,” akaeleza alipoulizwa sababu yake ya kuirejelea serikali hivyo.

  • Tags

You can share this post!

Jinsi mauaji chakani Shakahola yalivyoshtua ulimwengu

Wezi wavunja nyumba za walioenda mashambani kuenjoi

T L