• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 9:55 AM
Hofu PAA itakoroga UDA Pwani katika nyadhifa nyingi

Hofu PAA itakoroga UDA Pwani katika nyadhifa nyingi

NA VALENTINE OBARA

UAMUZI wa Chama cha Pamoja African Alliance (PAA) kujiunga na Muungano wa Kenya Kwanza, unatarajiwa kuibua vita vya ubabe baina ya wanasiasa wa Pwani wanaoegemea muungano huo.

Chama hicho kinachoongozwa na Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi, kilipokewa na kinara wa Kenya Kwanza, Naibu Rais William Ruto, anayeongoza Chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Bw Kingi alichukua hatua hiyo licha ya kuwa PAA ilichapishwa kwenye gazeti la serikali kama chama tanzu cha Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya mwezi uliopita.

Kabla ya PAA kuingia Kenya Kwanza, wanasiasa wanaoegemea UDA eneo la Pwani hawakuwa na ushindani mkubwa kutoka kwa vyama vya ndani ya muungano huo.

Walitumia nafasi hiyo kutangaza UDA kuwa ndicho chama kinachojali maslahi ya Pwani wakidai wao pia ni waanzilishi wake.

Vinara wa Kenya Kwanza katika ukanda huo wanajumuisha Gavana wa Kwale, Bw Salim Mvurya, aliyekuwa seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar, mbunge wa Nyali, Bw Mohamed Ali na mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa.

Kati ya wanasiasa hao, Bi Jumwa pekee ndiye alionekana katika kikao cha kupokea PAA ndani ya Kenya Kwanza jijini Nairobi.

Ijapokuwa PAA haikusimamisha mgombeaji urais, chama hicho kina wagombeaji viti mbalimbali vya kisiasa kote Pwani kuanzia ugavana hadi udiwani.

Dalili za mivutano inayotarajiwa zilishuhudiwa Jumanne, wakati Bw George Kithi, ambaye ni mgombeaji ugavana Kilifi kupitia kwa PAA, aliponyimwa nafasi ya kusimama karibu na Dkt Ruto.

Bi Jumwa, ambaye ndiye mgombeaji ugavana wa Kilifi kupitia UDA, alikuwa amealikwa kusimama karibu na Dkt Ruto pamoja na Bw Kingi na vinara wengine wa Kenya Kwanza.

Hata hivyo, Bw Kithi alipokaribia sehemu hiyo, mbunge wa Garissa Mjini, Bw Aden Duale, ambaye ni mshirika mkubwa wa UDA, alimvuta kando na kumlazimu kusimama pembeni.

Dkt Ruto aliashiria uwezekano wa mashauriano kati ya UDA na PAA kuhusu ushirikiano kuwania baadhi ya viti katika kaunti za Pwani.

“Jumwa na Kithi wamechangia sana kwetu kuja pamoja. Kuna maelewano kuhusu vile tutaenda mbele. Sasa tumeamua sisi ni kitu kimoja na tutajipanga pale ndani,” akasema Naibu Rais.

Katika Kaunti ya Mombasa, Bw Omar ndiye mgombeaji ugavana kupitia UDA, huku Naibu Gavana, Dkt William Kingi, akiipeperusha bendera ya PAA.

Kwingineko Kwale, UDA ilimsimamisha Naibu Gavana, Bi Fatuma Achani, huku PAA ikiwa na Bw Lung’anzi Chai.

Gavana Salim Mvurya amekuwa mstari wa mbele kumpigia debe naibu wake kurithi kiti hicho.

Katika hotuba yake, Bw Kingi alisisitiza kuwa, uamuzi wa kujiunga na Dkt Ruto ni kwa minajili ya kutimiza maendeleo Pwani na wala si kutafuta makubaliano kuhusu ugavi wa mamlaka.

Alisema chama chake kitajitahidi kumletea Dkt Ruto ushindi wa urais, lakini akatoa ilani kusiwe na hali ya kukoseana heshima katika muungano huo.

“Tumetoka mahali ambapo hapakuwa na uaminifu, kulipokuwepo udanganyifu wa kisiasa na natumai hatutaupata huku. Twatumai heshima na uaminifu utadumu katika muungano huu,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

CECIL ODONGO: Ruto hafai kukosoa chochote kuhusu SGR sababu...

‘Umenisaliti’, Raila amwambia Kingi

T L