• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:55 AM
CECIL ODONGO: Ruto hafai kukosoa chochote kuhusu SGR sababu alikuwa serikalini maamuzi yakifanywa

CECIL ODONGO: Ruto hafai kukosoa chochote kuhusu SGR sababu alikuwa serikalini maamuzi yakifanywa

NA CECIL ODONGO

NI kinaya kwa Naibu Rais, Dkt William Ruto kukosoa uchukuzi wa mizigo kutoka Bandari ya Mombasa hadi Nairobi na Naivasha kutumia reli ya kisasa ya SGR ilhali amekuwa hapo awali akijinadi kuwa alimsaidia Rais Uhuru Kenyatta kufaulisha mradi huo.

Dkt Ruto akimlaki Gavana wa Kilifi Amason Kingi katika Muungano wa Kenya Kwanza Jumanne, alikosoa hatua ya serikali kukumbatia uchukuzi wa mizigo kupitia SGR.

Mizigo inayofarishwa kupitia reli hiyo ya kisasa hufikishwa katika kituo cha makontena cha Embakasi na bandari kavu ya Naivasha.

Alidai uchukuzi huo umelemaza uchumi wa Pwani ambao kwa kiasi kikubwa hujizolea mapato na ajira kutokana na shughuli zinazoendelea katika bandari ya Mombasa.

Kwanza, serikali ilipoanza kutumia SGR kusafirisha mizigo mnamo Juni 2017, Dkt Ruto akiwa pamoja na Rais Uhuru Kenyatta kwenye kampeni ya kisiasa Pwani hakukosoa mradi huo.

Je, ni kipi kimebadilika ama sasa ni wakati wa kutumia suala hilo kujizolea kura za Wapwani?

Pili, wakati usafirishaji huo ulipoanzishwa Dkt Ruto hakuwa amekosana na Rais Kenyatta na usemi wake kuhusu masuala ya kitaifa ulikuwa ukizingatiwa sana katika baraza la mawaziri.

Kwa nini wakati huo hakuibua masuala anayoyazungumzia kwa sasa alipotambua kuwa mradi huo ulitekwa nyara kuwanufaisha watu wachache serikalini.

Ukweli ni kuwa usafiri huo wa mizigo kupitia SGR umevuruga uchumi wa Pwani na kusababisha kupotea kwa nafasi nyingi za ajira.

Katika mojawapo ya mikutano ya kisiasa Pwani 2017, Dkt Ruto aliandamana na Rais eneo la Voi ambako alisema bandari kavu itajengwa mji huo ili kusaidia kupunguza msongamano katika bandari ya Mombasa.

Wakati huo hakupinga kauli ya Rais japo alifahamu vyema kuwa hata SGR inayotumika kusafirisha mizigo Nairobi na Naivasha bado ndiyo ingetumika hadi Voi.

Nia nayo bado ilikuwa ile ile ya kupunguza msongamano huo huo bandari ya Mombasa.

Naibu Rais anafaa kufahamu kuwa Wakenya wana hekima na wamekuwa wakifuatilia miradi ya serikali kwa makini na si rahisi kuwapumbaza kama zamani.

Kilichoko ni kuwa kati ya 2013-2017, Dkt Ruto alihusika katika kufungua na kutekeleza miradi mingi ya serikali na hafai kumlaumu Rais au serikali ila wote wanafaa wabebe lawama kuhusu kasoro au dosari iliyotokea.

  • Tags

You can share this post!

Ndoto ya bondia Ongare kupata taji yasambaratika

Hofu PAA itakoroga UDA Pwani katika nyadhifa nyingi

T L