• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
‘Umenisaliti’, Raila amwambia Kingi

‘Umenisaliti’, Raila amwambia Kingi

NA VALENTINE OBARA

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, amemsuta Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi, kwa kuungana na mrengo wa Naibu Rais William Ruto.

Akizungumza leo Alhamisi akiwa Kilifi, Bw Odinga alisimulia jinsi alivyomshika mkono gavana huyo tangu alipokuwa limbukeni kisiasa, hadi akawa gavana kwa vipindi viwili.

“Kingi amenifanyia kitndo cha usaliti. Alipokuwa amemaliza masomo nilimbeba nikampeleka eneo la Gongoni, nikainua mkono wake. Wakati huo, Mbunge wa Magarini alikuwa ni Bw Harrison Kombe. Wakati huo Kombe alikuwa ameteleza akaenda upande wa Kibaki, nikasema huyo kijana Kingi ndiye ametosha. Alipigiwa kura kwa wingi kwa sababu alikuwa mrengo wangu. Alipokuwa mbunge nilimfanya waziri katika serikali yetu ya mseto. Nilikuwa namjua Hassan Joho kumshinda yeye lakini kwa sababu tulikuwa tayari tumemweka Najib Balala waziri kutoka Mombasa, tuliamua kumpa Kingi kutoka Kilifi. Alikuwa limbukeni bado. Tulipoingia ugatuzi aliniambia anataka kujaribu mambo ya ugavana. Nikatembea naye kote kusema huyu ndiye mtu wetu, akachaguliwa. Kufika 2017 tukakuja kusema Kingi tano tena. Akaenda tena lakini akaanza kutuambia Wapwani sasa hawataki ODM. Ati wanataka chama chao ili wawe kwenye meza wawe na sauti yao huko. Tulikaa naye na Joho na Junet tukiongea saa sita usiku akasema mambo yamebadilika, watu wetu wanataka wawe na sauti kitaifa kwa chama chao. Akaleta hii kitu inaitwa PAA. Sasa akileta baada ya kuleta PAA tena anaingia nayo Azimio kupitia kwa Jubilee, sio kupitia kwetu. Niliona hii ni kama bibi anataka kukuacha anaanza kupitia kwa mashemeji. Ametoroka peke yake akaenda kwa adui yetu. Roho yake ilikuwa huko. Amenipa mateke ya punda. Sasa nataka nyinyi watu wa Kilifi mumpe kichapo kuliko yale mateke ya punda.”

Bw Kingi, ambaye alishinda ugavana mara mbili kupitia kwa ODM, aliongoza chama chake cha Pamoja African Alliance (PAA) kujiunga na Muungano wa Kenya Kwanza mapema wiki hii.

Alidai kuwa, vinara wa Azimio hawakuonyesha nia ya kutimiza matarajio ya PAA kuhusu maendeleo ya Pwani kwani mambo yalikuwa yakifanywa kisiri.

Hata hivyo, viongozi wa ODM wakiongozwa na Bw Odinga wamedai hatua yake ni ya kufuata masilahi ya kibinafsi.

Mkataba wa Kenya Kwanza ulionyesha kuwa, Bw Kingi ameahidiwa kupewa wadhifa wa spika wa seneti iwapo atafanikiwa kumletea Dkt Ruto asilimia 50 ya kura za Kilifi za urais katika uchaguzi wa Agosti.

  • Tags

You can share this post!

Hofu PAA itakoroga UDA Pwani katika nyadhifa nyingi

‘Muthama hataki kuwa katika jukwaa moja na Alfred...

T L