• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 7:02 PM
Huenda IEBC ikamwidhinisha Kalonzo kuwania urais kivyake

Huenda IEBC ikamwidhinisha Kalonzo kuwania urais kivyake

WALTER MENYA na SAMWEL OWINO

HUENDA kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka akaruhusiwa kuwania urais endapo hakutakuwa na agizo la mahakama kumzuia kuwania kiti hicho.

Duru katika mkutano wa makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), uliojadili suala hilo, zinasema kuwa tume hiyo inapanga kuzingatia hitaji la Sehemu ya 23 ya Sheria ya Uchaguzi kuhusu vigezo vya kumwidhinisha mtu kuwania urais.

Wagombeaji wa urais wanatarajiwa kuwasilisha stakabadhi zao za uteuzi kwa tume hiyo Mei 30 ili zikaguliwa kabla ya wao kuteuliwa rasmi kuwania kiti hicho katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Sehemu hiyo ya sheria ya uchaguzi inaorodhesha masharti ambayo mtu anayetaka kuwania urais anafaa kutimiza.

Kwa mfano mtu kama huyo anafaa kuwa mzawa wa Kenya na asiwe na uraia wa nchi nyingine. Mtu huyo awe amehitimu kuwania kiti cha ubunge, amesajiliwa kuwa mpiga kura, awe mwanachama wa chama cha kisiasa kilichosajiliwa au amejisajili kama mgombea huru, na sharti awe ameteuliwa na chama fulani cha kisiasa na cheti chake kutiwa saini na maafisa wanaokubaliwa kufanya hivyo.

Vile vile, mtu anayetaka kuwania urais sharti awe ameungwa mkono na angalau wapigakura 2,000 katika angalau kaunti 24, awe ni mtu ambaye hajawahi kutangazwa kuwa amefilisika, asiwe amehukumiwa kifungo cha miezi sita kuanzia wakati alipojiandikisha kama mwaniaji.

IEBC pia imeandaa mkutano na wawaniaji urais au wawakilishi wake Jumatatu ijayo, ili kuwajuza kuhusu yale wanayofaa kutimiza kuelekea siku ya uteuzi Mei 30.

Mkutano huo utafanyika katika ukumbi wa Bomas of Kenya, Nairobi.

Katika mazungumzo hayo ya makamishna wa IEBC, uanachama wa mtu katika muungano fulani sio mojawapo ya masuala yanayoweza kuathiri nafasi ya mtu kuruhusiwa kuwania urais.

Hii ina maana kuwa IEBC itamwidhinisha Bw Musyoka kuwania urais, licha ya kwamba chama chake cha Wiper ni moja ya vyama tanzu katika muungano wa Azimio la Umoja –One Kenya.

Muungano huo, ambao pia umesajiliwa kama chama cha kisiasa, umemwidhinisha Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kama mgombeaji wake wa urais katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

“Mradi ametimiza mahitaji kuhusu uteuzi wa wawaniaji urais, ataidhinishwa,” afisa mmoja aliyeshiriki katika mpango wa kuandaa ushauri kuhusu suala hilo, aliambia Taifa Leo.

“Hii ni kwa sababu afisa wa kusimamia uchaguzi anayehusika na uchaguzi wa urais huwa haketi katika kamati ya kutatua mizozo,” afisa huyo akaongeza.

Hata hivyo, ikiwa mtu yeyote atapinga hatua ya Bw Musyoka kuwania urais, baada ya IEBC kumwidhinisha, tume hiyo itabuni Kamati ya Kutatua Mizozo kuchunguza suala hilo.

Kiongozi huyo wa Wiper na wandani wake wameshikilia kuwa atawania urais baada ya kujiondoa katika Azimio.

Hii ni baada ya mwaniaji urais wa muungano huo, Bw Raila kutomteua kuwa mwaniaji mwenza wake na badala yake kumteua kiongozi wa Narc Kenya katika nafasi hiyo.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Kongole kwa mashujaa wetu waliofana Brazil

Sababu za Karua kukwepa Uhuru

T L