• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Sababu za Karua kukwepa Uhuru

Sababu za Karua kukwepa Uhuru

NA LEONARD ONYANGO

MWANIAJI mwenza wa urais wa Azimio la Umoja-One Kenya, Bi Martha Karua, amekuwa akikwepa kuimiminia sifa serikali ya Rais Uhuru Kenyatta katika msururu wa kampeni zake eneo la Mlima Kenya.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa Bi Karua ambaye ni mwaniaji mwenza wa urais wa Bw Raila Odinga, anakwepa kuupaka tope muungano wa Azimio mbali na kuusawiri kama mradi wa serikali.

Bi Karua alianza ziara ya kumnadi Bw Odinga katika eneo la Mlima Kenya siku moja baada ya kutangazwa kuwa mwaniaji mwenza katika jumba la KICC, Nairobi, Jumatatu.

Rais Kenyatta ambaye ni mwenyekiti wa Baraza Kuu la Azimio, hakuhudhuria hafla ya kumtawaza Bi Karua kuwa mwaniaji mwenza wa Bw Odinga – hatua ambayo wadadisi wanasema ililenga kutoa taswira kwamba waziri mkuu huyo wa zamani alimteua kinara wa Narc Kenya bila ushawishi wa Ikulu.

Jana Ijumaa, Bi Karua alikuwa katika Kaunti za Murang’a na Nyeri ambapo alihutubia wakazi katika maeno mbalimbali, ikiwemo Mathira ambalo ni eneobunge la Bw Rigathi Gachagua, mwaniaji mwenza wa urais wa Naibu wa Rais William Ruto.

Leo Jumamosi, msafara wa Bi Karua ambaye ameandamana na waziri wa Kilimo, Peter Munya, umekuwa katika Kaunti ya Kiambu kabla ya kuelekea jijini Nairobi kesho Jumapili ambapo atazuru maeneo yaliyo na idadi kubwa ya wakazi kutoka eneo la Mlima Kenya.

Jumatatu, Bi Karua atapumzika huku Jumanne na Jumatano akielekea katika Kaunti za Laikipia na Nyandarua mtawalia.

Wanasiasa wa muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Dkt Ruto wamekuwa wakishutumu Rais Kenyatta kwa kutelekeza wakazi wa Mlima Kenya wakati wa ungozi wake.

Bw Javan Bigambo anasema kuwa Bi Karua huenda akabeba mabaya ya serikali ya Jubilee iwapo ataanza kumsifia Rais Kenyatta kwenye kampeni zake eneo la Mlima Kenya.

“Mabaya ya serikali ya Jubilee yamemwathiri zaidi Bw Odinga ambaye amekuwa mshirika wa karibu wa Rais Kenyatta tangu 2018. Bi Karua huenda akajipata katika mtego huo ikiwa ataanza kummiminia sifa Rais Kenyatta,” akasema Bw Bigambo.

Anasema kuwa hatua ya Bi Karua kujitenga na serikali ya Jubilee itamfanya kuwa ‘mwokozi wa kisiasa’ wa Bw Odinga katika eneo Mlima Kenya.

Prof Masibo Lumala wa Chuo Kikuu cha Moi anasema Bi Karua amewavutia wengi kutokana na sifa yake ya uadilifu hivyo basi itakuwa hatari kujipaka tope kwa kuanza kusifia mema ya serikali ya Rais Kenyatta hasa katika eneo la Mlima Kenya.

“Ingawa hajatambuliwa kuwa kinara wa kisiasa wa eneo la Mlima Kenya, Bi Karua amejizolea sifa za kuwa kiongozi mwenye maadili mema. Sifa hiyo itamwezesha kumletea Bw Odinga kura nyingi,” anasema Prof Lumala.

Katika hotuba zake, Bi Karua amekuwa akimsifia Bw Odinga akimtaja kama mtetezi wa wanyonge na mchapakazi.

“Michoro yake alipokuwa waziri wa Miundomsingi wakati wa serikali ya ‘nusu mkate’ chini ya Rais Mwai Kibaki (kati ya 2008 na 2013) ndiyo inayotumiwa hadi sasa kujenga barabara. Kazi yake nzuri ilimfanya kutambuliwa na akateuliwa kuwa Balozi wa Miundomsingi wa Umoja wa Afrika,” akasema Bi Karua alipokuwa akihutubia Ijumaa wakazi wa eneo la Othaya, Kaunyi ya Nyeri.

Bi Karua pia amekuwa akiwahakikishia wakazi wa Mlima Kenya kuwa atakabiliana na ufisadi ambao unaonekana kushika kasi ndani ya serikali ya Jubilee.

Mbunge wa Gatanga Joseph Nduati ambaye ni mtetezi mkuu wa Rais Kenyatta, anasema kuwa Bi Karua atatumia ushawishi wake wa kisiasa alio nao sasa kuunganisha wakazi wa Mlima Kenya kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kampeni za Bw Odinga na Gavana wa Laikipia Ndiritu Muriithi pia anaonekana kukiri kuwa Bi Karua huenda akaokoa Bw Odinga katika eneo la Mlima Kenya kwa kumsaidia kupata kura nyingi.

  • Tags

You can share this post!

Huenda IEBC ikamwidhinisha Kalonzo kuwania urais kivyake

Kundi lataka wandani wa Raila na Ruto wazuiwe kugombea vyeo...

T L