• Nairobi
  • Last Updated May 14th, 2024 10:01 PM
IEBC yampa Kalonzo muda wa hadi Jumapili Mei 29 kuwasilisha stakabadhi kwa mfumo sahihi

IEBC yampa Kalonzo muda wa hadi Jumapili Mei 29 kuwasilisha stakabadhi kwa mfumo sahihi

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka amepata afueni ya muda katika juhudi zake za kuidhinishwa kuwania urais baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kumpa mwanya wa hadi Jumapili, Mei 29, 2022 kuwasilisha stakabadhi zake kwa mfumo sahihi.

Kwenya barua ambayo mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati aliandikia Wiper na ambayo Taifa Leo ilipata nakala yake, chama hicho kimetakiwa kuwasilisha stakabadhi hizo kwa mfumo sahihi kufia saa tatu za asubuhi katika ukumbi wa Bomas, Nairobi.

“Tume hii imekubaliana na ombi lenu kwamba mruhusiwe kuwasilisha sahihi za wafuasi kwa mfumo wa Microsoft Excel Sheet kufikia Mei 29, 2022 saa tatu za asubuhi katika ukumbi wa Bomas of Kenya. Mkifeli kufanya hivyo, stakabadhi zenu zitakataliwa kwa kufeli kuzingatia sheria iliyowekwa,” akasema Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati katika barua hiyo.

Hii ni baada ya kubainika kuwa chama cha Wiper kiliwasilisha orodha ya sahihi za watu 2,000 kutoka angalau kaunti 24 wanaounga mkono azma ya urais ya Bw Musyoka kwa mfumo wa PDF badala ya ule wa Microsoft Excel inavyohitaji.

Hii ni kulingana na kanuni 18 ya Sheria ya Uchaguzi 2016 kuhusu masharti yanayofaa kuzingatiwa na wawaniaji urais kabla ya kuidhinishwa na IEBC kuidhinisha kushiriki kinyang’anyiro hicho.

Mnamo Ijumaa, Mei 27, 2022 IEBC ilisema Bw Musyoka hangeruhusiwa kuwania urais kwa tiketi ya Wiper, kwa sababu sahihi za na nakala za vitambulisho vya kitaifa vya wanaounga azma yake haziwasilishwa kwa mfumo hitajika.

Hayo yanajiri wakati ambapo wandani wa Bw Musyoka, kama vile Naibu Mwenyekiti wa Wiper Mutula Kilonzo Junior, wakishikilia kuwa mwanasiasa huyo yu njia kurejea muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya.

Akiongea katika mkutano wa kampeni katika eneo la Kisau, kaunti ya Makueni Ijumaa Seneta huyo wa Makueni alisema kuwa Bw Musyoka atafanya mazungumzo na uongozi wa Azimio ili kukubaliana kuhusu nyadhifa ambazo zitatengewa Wiper endapo muungano huo utashinda katika uchaguzi mkuu.

Bw Kilonzo Junior alikariri kuwa Bw Musyoka yu tayari kumuunga mkono mgombea urais wa Azimio, Raila Odinga, “japo Wiper ilidhulumiwa kwa kunyimwa nafasi ya mgombea mwenza.”

  • Tags

You can share this post!

Wanga ajiondoa lawamani mgomo wa wahudumu

Wafalme Ogier na Loeb kunogesha Safari Rally iliyoshuhudia...

T L