• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
JAMVI: Je, Ruto amegeuka kiongozi wa upinzani?

JAMVI: Je, Ruto amegeuka kiongozi wa upinzani?

Na CHARLES WASONGA

KWA mara si moja Naibu Rais William Ruto amekuwa akiwakumbusha Wakenya kwamba yeye ndiye Naibu Rais wa Kenya na ni “mtu wa mkono” wa Rais Uhuru Kenyatta anayemtuma kila mara kumwakilisha katika ziara zake za kuzindua na kukagua miradi ya maendeleo kote nchini.

Lakini kinaya ni kwamba tangu Machi 9 mwaka jana, Rais Kenyatta alipozika uhasama wake wake kisiasa na kiongozi wa ODM Raila Odinga, amekuwa akienda kinyume na misimamo ya mkubwa wake, hali inayomfanya kuonekana kama “mwanasiasa wa upinzani”.

Hii ni kwa sababu tangu hapo, Dkt Ruto na wabunge wa Jubilee wanaounga mkono azma yake ya kuwa Rais 2022, wameonekana wakipinga misimamo na kukaidi maagizo na baadhi ya sera serikali ambazo wanapaswa kuunga na pia kuzitetea.

Isitoshe, katika mkutano wa hadhara ambao ulioongozwa na Naibu Rais katika eneo bunge la Endebess, kaunti ya Trans Nzoia kundi la wabunge hao maarufu kama “Team Tanga Tanga” walimtaka Waziri Fred Matiang’i kujiuzulu kuhusiana na sakata ya dhahabu feki, la sivyo wamfurushe.

Wadadisi wa masula ya utawala na uongozi wanasema ili ni makosa kwa Dkt Ruto hatomtetea Dkt Matiang’i chini ya moyo wa wajibu wa pamoja unaowashikanisha maafisa wa serikali, hususan wanachama wa baraza la mawaziri.

“Ikiwa kweli yeye ni Naibu Rais, wala sio mwanasiasa wa upinzani, ilikuwa wajibu wake kuwakemea wabunge hao kama vile Aisha Jumwa na kuwakumbusha kuwa Matiang’i ni afisa wa serikali anayoongoza pamoja na mkubwa wake, Rais Kenyatta,” akasema Bw Barasa Nyukuri ambaye ni mtaalamu katika masuala ya uongozi na utawala.

“Dkt Ruto hapaswi kuacha maslahi yake ya kisiasa kumfanya asahau kwamba yeye ni mhusika katika serikali ya hii na hafai kuonekana kuipinga kwa kunyamaza wanasiasa wanapomponda afisa wake kuhusu suala ambalo bado linachunguzwa,” akaongeza.

Vilevile, Naibu Rais ametangaza bayana kwenye mahojiano katika vyombo vya habari na katika mikutano ya hadhara kwamba haungi mkono muafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kwa sababu kiongozi huyo wa ODM “sio mtu wa kuaminika.”

Kulingana na Dkt Ruto nia hasa ya Bw Odinga katika muafaka huo ni kusambaratisha Jubilee na kuzika ndoto yake ya kumrithi mkubwa wake, Rais Uhuru Kenyatta.

Hii ni tofauti na Rais Kenyatta ambaye amekariri mara kadha kwamba amesimama imara nyuma ya muafaka huo maarufu kama handisheki ambao alisema unalenga kupalilia amani, umoja na utangamano nchini.

“Mimi hushauriana na ndugu yangu Raila mara kwa mara. Na mazungumzo yetu yamelenga kuliunganisha taifa hili wala sio siasa za urais. Raila hajawahi kuniambia kuwa anataka kuwania urais 2022 na mimi sijamwambia nataka kuendelea kuwa uongozini baada ya 2022. Wale wanaeneza uvumi kama huo kila mara wanapaswa kutafuta kitu kingine cha maana kufanya,” Rais Kenyatta akasema mwezi jana katika ukumbi wa Bomas, katika mkutano kuhusu miundomsingi ambao uliongozwa na Bw Odinga.

Itakumbukwa kwamba, mnamo Juni mwaka jana Dkt Ruto na wandani wake walipinga waziwazi amri ya Rais Kenyatta kwamba hali ya maisha ya watumishi wa umma yanakaguliwa kubaini asili ya utajiri wao.

Akiongea alipokuwa akikagua miradi ya barabara katika eneo la pwani, kiongozi wa taifa alisema zoezi hilo litakuwa hatua mojawapo ya kupambana na zimwi la ufisadi katika sekta ya umma ambayo imekuwa ikiiharibia sifa serikali.

“Tunaendesha ukaguzi wa hali ya maisha ya watumishi wote wa umma kuanzia mimi kisha huyu (Dkt Ruto) kabla ya kuendeleza shughuli hiyo katika ngazi za utumishi wa umma. Tunafanya hivi kama sehemu ya vita dhidi ya ufisadi,” akasema huku akiwa ameandama na naibu wake na viongozi kadha, akiwemo Gavana wa Mombasa Hassan Joho.

Rais Kenyatta alisema wakati wa shughuli hiyo ambayo ilipaswa kuanza Julai 1, 2018, watumishi wote wa umma watahitajika kuelezea asili ya mali yao na wale watakaopatikana kosa la wizi wa pesa za umma watawajibishwa na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

Lakini kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Kipchumba Murkomen, Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi walipiga agizo hilo la Rais Kenyatta wakisema hiyo ilikuwa njama ya kumpaka tope Dkt Ruto na kumsawiri kama kiongozi fisadi.

“Hatuamini hii shughuli hata kidogo na tunaipinga kabisa. Hii ni njama ya kumharibia sifa Naibu Rais na kwa kumsingizia tuhuma za ufisadi ili kuzima ndoto yake ya kuingia Ikulu 2022. Ikiwa ukaguzi huo utafanywa sharti na familia ya Kenyatta ifanyiwe ili Wakenya wajue asili ya mali yangu kuanzia mwaka wa 1963 hadi sasa,” akasema Bw Sudi.

Naye Bw Murkomen alishikilia kuwa hakuna mfumo faafu wa sheria ambao ulipaswa kulinda kuongoza shughuli hiyo akielezea hatari ya amri hiyo kutumiwa kuendeleza njama za kuwaharibia jina watumishi wa umma wasio na hatia.

Na mwezi Machi mwaka huu Dkt Ruto alitofautiana hadharani kuhusu vita dhidi ya ufisadi haswa uchunguzi kuhusu sakata ya wizi wa Sh21 bilioni pesa zilizonuiwa kufadhili ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer katika kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Akihutubu katika majengo ya Mahakama ya Juu, Nairobi akiandamana na naibu wake, Rais aliunga mkono utendakazi wa mkurugenzi wa upelelezi wa jinai George Kinoti katika uchunguzi wa sakata hiyo.

Lakini kwa upande wake Dkt Ruto alienda kinyume na msimamo wa Rais kwanza kwa kudai Bw Kinoti alidanganya kuwa ni Sh21 bilioni zilizopotea ilhali, kulingana naye ni Sh7 bilioni pekee ambazo “zilitumika visivyo.”

Siku chache, baadaye Dkt Ruto alitumia jukwaa la kisiasa katika eneo bunge la Ainamoi, kaunti ya Kericho kumponda Bw Kinoti akidai kuwa ameingiza siasa katika vita dhidi ya ufisadi kwa kulenga watu kutoka jamii yake pekee.

Dkt Nyukuri anamshauri Dkt Ruto kuunga mkono misimamo na maongozi ya serikali ya Jubilee, pasina kuonekana “kupinga kila kitu” ikiwa anapania kufaulu katika ndoto yake ya kumrithi Rais Kenyatta mnamo 2022.

You can share this post!

JAMVI: Wanasiasa wakongwe Mlima Kenya waanza kujifufua...

Waziri wa zamani aliyeponea kifo 1994 afariki jijini Nairobi

adminleo