• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Waziri wa zamani aliyeponea kifo 1994 afariki jijini Nairobi

Waziri wa zamani aliyeponea kifo 1994 afariki jijini Nairobi

NA GAITANO PESA 

WAZIRI Msaidizi wa zamani Fredrick Oduya Oprong alifariki Jumapili Mei 26 katika Hospitali Kuu ya Kenyatta jijini Nairobi akiwa na umri wa miaka 83.

Marehemu ambaye pia alihudumu kama mbunge wa Amagoro, eneobunge ambalo sasa limegawanywa kuwa Teso Kusini na Teso Kaskazini, alikuwa waziri msaidizi katika Wizara ya Mipango ya Kiuchumi na Maendeleo ya Kitaifa kwenye serikali ya Rais Mstaafu Daniel Arap Moi.

Mnamo mwaka wa 1994, Bw Oprong nusura apoteze maisha yake alipopigwa risasi mbili kichwani na watu wasiojulikana jijini Nairobi.

Tangu wakati huo, mwanasiasa huyo amekuwa akiishi akiwa na risasi moja kichwani baada ya madaktari kuondoa moja na kuacha nyingine kwa kuwa ilikuwa hatari na ingechangia kifo chake.

Gavana wa Busia Sospeter Ojaamong alikuwa wa kwanza kutuma risala ya rambirambi kwa familia ya marehemu akisema alilikweza mno jina la eneo la Teso kwenye siasa za kitaifa kabla na baada ya Kenya kupata uhuru.

“Kaunti yetu imepoteza kiongozi ambaye aliongoza ujumbe wa wazee kwa kamishina wa serikali ya mkoloni ili kupigania kubuniwa kwa eneobunge la Busia Kaskazini ambalo baadaye lilizaa maeneobunge mengine tuliyonayo leo,” akasema Bw Ojaamong.

Gavana huyo aliongeza kwamba ni marehemu aliyechangia ziara ya kwanza ya Rais Jomo Kenyatta eneo hilo baada ya kuachiliwa kutoka gerezani mwaka wa 1961.

“Mzee Oduya alikuwa kati ya viongozi wa kwanza kutoka Magharibi mwa Kenya kukutana na Mzee Kenyatta baada ya kuachiliwa kwake mwaka wa 1961. Mkutano huo ndio ulikuwa kichochea cha Mzee Kenyatta kuandaa mkutano wa wa kwanza wa kisiasa katika mpaka wa Malaba, Magharibi mwa Kenya.

“Kifo kimetupokonya mwanasiasa ambaye alichangia kuandikwa kwa katiba ya kwanza ya Kenya. Uhusiano wake wa karibu na familia za Mzee Kenyatta na Jaramogi Oginga Odinga umesaidia sana kizazi cha sasa cha jamii ya Teso,” akaongeza Gavana huyo.

Imetafsiriwa na na CECIL ODONGO

You can share this post!

JAMVI: Je, Ruto amegeuka kiongozi wa upinzani?

Ajikata nyeti na kuzihifadhi kwa jokofu

adminleo