• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:55 AM
JAMVI: Presha ya ‘Tangatanga’ yamzidia Uhuru

JAMVI: Presha ya ‘Tangatanga’ yamzidia Uhuru

Na LEONARD ONYANGO

MKUTANO baina ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto, wiki iliyopita ulichukuliwa ulilenga kukomesha malumbano kati ya makundi mawili katika chama cha Jubilee.

Hata hivyo kundi linalomuunga Bw Ruto limeendelea kumkosoa kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga katika kile wadadisi wanasema ni kumshinikiza Rais Kenyatta kuvunja muafaka ambao ulituliza nchi.

Hata baada ya Rais Kenyatta, kumtembelea Bw Ruto ofisini na kula chamcha naye, hali haijabadilika huku wandani wa Ruto katika kundi la Tanga Tanga wakiendelea kuwashambulia wenzao katika Jubilee na Bw Odinga.

Wadadisi wanasema lengo ni kumpa presha Rais Kenyatta aachane na Bw Odinga, vita dhidi ya ufisadi na kuheshimu makubaliano yake na Bw Ruto kwamba atamuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Kabla ya mkutano huo, Kiongozi wa Wengi Bungeni Aden Duale alikuwa amemtaka Rais Kenyatta kukutana na wabunge wa Jubilee kabla ya kuhutubia Bunge la Kitaifa Aprili 4, mwaka huu.

Kulingana na Bw Duale ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto, mkutano huo ungesaidia kuunganisha viongozi wa chama tawala cha Jubilee ambao sasa wamegawanyika katika makundi mawili.

Kundi la wanasiasa wanaounga azma ya Dkt Ruto ya kuwania urais 2022, linapinga vita dhidi ya ufisadi. Kulingana na Bw Ruto pamoja na wanasiasa wanaoegemea upande wake, vita dhidi ya ufisadi vinavyoendelea vinalenga kusambaratisha azma yake ya kutaka kumrithi Rais Kenyatta anayetarajiwa kustaafu 2022.

Kambi ya Ruto pia inataka Rais Kenyatta kutengana na kiongozi wa ODM Raila Odinga wanayedai analenga kubomoa chama cha Jubilee.

Kwa upande, mwingine Rais Kenyatta anasisitiza kuwa hatalegeza kamba katika vita dhidi ya ufisadi na kuunganisha Wakenya.

Vita dhidi ya ufisadi na juhudi zake za kutaka kuunganisha Wakenya ni miongoni mwa masuala ambayo Rais Kenyatta anatarajiwa kuangazia katika hotuba yake ya Alhamisi.

Hii ni mara ya pili kwa Rais Kenyatta kuhutubia Bunge la Kitaifa tangu kusalimiana na kukubali kushirikiana na Bw Odinga mnamo Machi, mwaka jana.

Mkutano wa wiki iliyopita baina ya viongozi hao wawili unaonekana kutuliza joto katika chama cha Jubilee kufuatia Bw Duale kubadili msimamo wake kwa kusema kuwa hakukuwa na haja ya Rais Kenyatta kukutana na wabunge wa Jubilee.

“Hakuna haja ya wabunge wa Jubilee kukutana na Rais Kenyatta kwani hakuna tofauti kati yetu,” Bw Duale alinukuliwa akisema Jumatano iliyopita.

Japo masuala yaliyojadiliwa na viongozi hao hayakuwekwa wazi, duru zinasema kuwa Rais Kenyatta alimtaka Dkt Ruto kuwanyamazisha wanasiasa wa kambi yake ambao wamekuwa wakipinga juhudi za kukabiliana na ufisadi.

Ni katika mkutano huo, ambapo inaaminika Rais Kenyatta aliweka wazi kwamba hayuko tayari kukutana na wabunge wa Jubilee.

Hata hivyo, wabunge wanaomuunga Bw Ruto walizidisha malumbano kwa kukosoa vita dhidi ya ufisadi na muafaka wakisema unalenga kuvunja Jubilee.

Rais Kenyatta hajawahi kuitisha mkutano wa viongozi wa Jubilee tangu alipotangaza kushirikiana na Bw Odinga licha ya kuwepo na shinikizo la kutaka awaeleze mambo yaliyo katika mkataba wa handisheki.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa hatua ya Rais Kenyatta kuzuru ofisi ya naibu wake lilikuwa onyo fiche kwa wanasiasa wa chama cha ODM wakiongozwa na James Orengo wanaopanga kumtimua Dkt Ruto kutokana na madai ya kuhusika na ufisadi.

“Rais Kenyatta alimtembelea naibu wake siku moja tu baada ya Bw Orengo kutangaza kumtimua kupitia kura bungeni. Huenda ziara ya rais lilikuwa onyo kwa akina Orengo kwamba mpango huo utagonga mwamba,” anasema Wakili Felix Otieno.

Kadhalika, inadaiwa kuwa Rais Kenyatta alimtembelea naibu wake kighafla bila kumfahamisha.

Duru zinasema kuwa Rais Kenyatta alimpigia simu Dkt Ruto kumfahamisha kuwa angemtembelea afisini kwake wakati wa maakuli ya mchana.

Mhadhiri wa Siasa katika Chuo Kikuu cha Nairobi Edward Kisiang’ani anaunga mkono hoja hiyo huku akisema kuwa mkutano huo ulipangwa na wala haukuwa wa dharura.

“Kila dalili zinaonyesha kwamba mkutano kati ya Rais Kenyatta na naibu wake ulipangwa kwa sababu na wala hakuna dalili ya kuonyesha kwamba ulikuwa wa kushtukia tu,” anasema Prof Kisiang’ani.

Wanaoshikilia kwamba Rais Kenyatta alimtembelea naibu wake kwa kushtukia, wanadai kuwa kupatikana kwa baadhi ya wabunge wa kikosi cha Tanga tanga katika afisi ya Dkt Ruto ni ishara kwamba hawakufahamu kwamba rais angetokea wakati huo siku hiyo.

Inadaiwa kuwa naibu wa rais alikuwa akikutana na wanasiasa wa kambi yake, akiwemo wabunge Aisha Jumwa (Malindi) na Benjamin Washiali (Mumias Mashariki) kabla ya Rais Kenyatta kuwasili.

You can share this post!

JAMVI: Muungano wa Isaac Ruto na Gideon Moi ni hatari kwa...

JAMVI: Kushindwa kudhibiti Pwani ni dalili Joho hatoshi...

adminleo