• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
JAMVI: Suluhu atarudisha urafiki na majirani?

JAMVI: Suluhu atarudisha urafiki na majirani?

Na WANDERI KAMAU

BAADA ya kuchukua uongozi mpya wa Tanzania kufuatia kifo cha Rais John Pombe Magufuli, kibarua kikubwa kinachomkabili rais mpya, Suluhu Hasssan, ni kurejesha uhusiano mzuri wa taifa hilo na majirani wake.

Licha ya kuwa maarufu sana miongoni mwa Watanzania, marehemu Magufuli amekuwa akikosolewa pakubwa kwa kutoweka juhudi za kutosha kuboresha uhusiano wa Tanzania na majirani wake, hasa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Kando na Tanzania, EAC ina nchi sita wanachama; miongoni mwazo zikiwa Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.

Kwa mujibu wa wadadisi wa siasa za ukanda huu, uhusiano baridi kati ya Magufuli na nchi hizo ulidhihirika Jumatano wakati wa misa yake ya wafu, kwani kando na Rais Uhuru Kenyatta, hakuna kiongozi mwingine wa mataifa hayo alihudhuria.

Marais wengine waliwatuma wawakilishi wao badala ya kuungana na Watanzania kumuaga kiongozi wao.

Marais Paul Kagame (Rwanda), Yoweri Museveni (Uganda), Salva Kiir (Sudan Kusini) na Evariste Ndayishimiye (Burundi) waliwakilishwa na mabalozi wao au wajumbe maalum waliowatuma kufikisha risala zao za rambirambi.

“Ni taswira iliyoonyesha kuwa Magufuli hakuwa kiongozi aliyetilia maanani ushirikiano wa kikanda na majirani wake,” asema Dkt Godfrey Sang, ambaye ni mchanganuzi wa siasa na mahusiano ya kimataifa.

Kulingana na mdadisi huyo, kibarua alicho nacho Rais Suluhu ni “kuirejesha Tanzania katika mwelekeo ufaao wa kikanda” kwani kwa sasa, taifa hilo halina utambulisho wowote kuhusu mwegemeo wake wa kikanda.

Anasema ni sababu hiyo ambapo kati ya viongozi waliohudhuria misa hiyo, wengi walitoka katika nchi za eneo la Kusini mwa Afrika.

Marais kutoka nchi za kusini mwa Afrika waliohudhuria hafla hiyo ni Filipe Jacinto-Nyusi (Msumbiji), Cyrus Ramaphosa (Afrika Kusini), Lazarus Chakwera (Malawi), Edgar Lungu (Zambia), Mokgweetsi Matsitsi (Botswana), Emmerson Mnangagwa (Zimbabwe), Hage Geingob (Namimbia) na Azali Assoumani (Visiwa vya Comoro).

Wadadisi wanasema ingawa hilo lilionyesha ukaribu ambao utawala wa Magufuli ulikuwa nao na nchi wanachana wa Jumuiya ya Maendeleo ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika (SADC), Tanzania haiwezi kustawi kiuchumi bila kushirikiana mataifa ya EAC.

“Ni dhahiri kuwa kwa muda mrefu, Tanzania imekuwa ikiegemea eneo la Kusini kwa masuala ya kibiashara na kiuchumi. Hata hivyo, kosa ambalo Magufuli alifanya ni kutotambua kuwa hawezi kujitenga na EAC, kwani ni nchi jirani na zinazotegemeanasana katika karibu kila nyanja,” asema Dkt Barrack Muluka, ambaye ni mchanganuzi wa siasa za kimataifa.

Kwa kipindi cha miaka sita ambayo aliitawala Tanzania, uhusiano wa Kenya na taifa hilo ulidorora sana, hasa katika ushirikiano wa kibiashara na mikakati ya kukabili janga la virusi vya corona.

Mnamo Novemba 2017, polisi wa Tanzania walichoma vifaranga 6,400 wenye umri wa siku moja pekee, wakidai walikuwa wameagizwa kutoka Kenya bila kufuata taratibu zifaazo za kisheria.

Tukio hilo lilizua taharuki kati ya mataifa hayo mawili, baadhi ya wafanyabiashara kutoka Kenya wakidai kuhangaishwa na maafisa wa usalama katika nchi hiyo.

Muda mfupi baada ya tukio hilo, maafisa wa usalama wa Tanzania walitwaa ng’ombe zaidi ya 1,300 kutoka wachungaji wa jamii ya Maasai kutoka Kenya, kwa kisingizio cha kulisha katika himaya ambayo hawakuwa wamekubaliwa.

Baadaye, waliwauza ng’ombe hao wote kama “adhabu” kwa wafugaji hao.

Akirejelea tukio hilo, Rais Magufuli alinukuliwa akisema kuwa “Tanzania si eneo la Wakenya kuwalishia ng’ombe wao.”

Uhusiano kati ya nchi hizo uliendelea kudorora, hasa kwenye mikakati ya kukabili maambukizi ya virusi vya corona.

Mnamo Novemba 2020 Tanzania ilipiga marufuku mashirika matatu ya ndege kutoka Kenya dhidi ya kuhudumu nchini humo, baada ya Kenya kuiorodhesha kuwa miongoni mwa nchi zisizo salama kutokana na virusi hivyo.

Tanzania haijakuwa ikitoa maelezo kuhusu kiwango cha maambukizi ya virusi hivyo tangu Aprili 2020.

Kama njia ya kulipiza kisasi, Mamlaka ya Safari za Ndege ya Tanzania (TCAA) ilipiga marufuku mashirika ya ndege ya AirKenya Express, Fly540 na Safarilink dhidi ya kuhudumu katika himaya yake.

Hali ilirejea shwari baada ya Kenya kulegeza masharti iliyokuwa imeweka kwenye mpaka wake.

Chini ya mazingira hayo, wadadisi wanasema jukumu kuu linalomkabili Rais Suluhu ni kuondoa uadui huo na dhana kwamba Tanzania ni taifa “lililojitenga” na washirika wake katika EAC.

“Haya ni mataifa jirani na yaliyo katika ukanda mmoja. Yanapakana na kutegemeana moja kwa moja. Hili ni jambo la dharura analopaswa kushughulikia,” asema Prof Macharia Munene, ambaye ni mhadhiri wa somo la Historia.

Anasema Magufuli aliibua dhana ya uhasama, iliojenga uadui ambao kamwe haufai kuwepo kati ya nchi jirani.

Anaeleza mwelekeo huo uliziathiri nchi zote, hasa katika masuala ya kibiashara na kukuza chumi zake.

You can share this post!

TAHARIRI: Kufungwa kaunti 5 kutaumiza wengi

Wanachama wa chama tawala cha Zimbabwe wadungwa chanjo ya...