• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 10:55 AM
JAMVI: Viunzi tele katika jitihada za Ruto kuvumisha UDA

JAMVI: Viunzi tele katika jitihada za Ruto kuvumisha UDA

Na CHARLES WASONGA

VUTA nikuvute miongoni mwa wabunge wanaoegemea chama cha United Democratic Alliance (UDA), kinachohusishwa na Naibu Rais William Ruto, huenda ikalemaza juhudi za kukiimarisha chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Jambo jingine linalotishia kuzima ndoto ya chama hicho kushinda katika uchaguzi huo ni kujivuta kwa baadhi ya wandani wa Dkt Ruto katika maeneo ya Magharibi mwa Kenya, Mlima Kenya na Pwani kushiriki moja kwa moja katika shughuli za chama hicho.

Wadadisi wanasema hizi ni miongoni mwa sababu zilichangia UDA kutangaza kuwa haiwadhamini wagombeaji katika chaguzi ndogo za ubunge wa Juja na useneta wa Garissa zitakazofanyika Mei 18 mwaka huu.

Hayo yanajiri wakati ambapo chama hicho kinajiandaa kufanya uchaguzi wa mashinani kuanzia Juni mwaka huu ambapo viongozi na washirikishi wake kuanzia ngazi ya wadi watachaguliwa.

Ni kutokana na misukosuko hii ambapo mnamo Jumatano, Dkt Ruto alifanya mkutano wa faragha na wabunge wandani wake na akawataka kukomesha vita na walenge kukiimarisha UDA kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2022.

“Ni kweli kwamba Naibu Rais alikutana nasi na kutuonya dhidi ya mivutano ambayo inaweza kuporomosha juhudi za UDA kutwaa uongozi wa taifa hili 2022. Haswa Dkt Ruto aliwataka viongozi kutoka Nakuru na North Rift kukomesha vita wakati huu ambapo chama kinajiandaa kwa uchaguzi wa mashinani,” Mbunge mmoja akaambia Taifa Jumapili.

“Vile vile, alituambia tusahau kabisa matokeo ya chaguzi za Matungu na Kabuchai ambapo wagombeaji wa UDA walishindwa na tuelekeze juhudi zetu katika kukiimarisha chama hiki,” akaeleza Mbunge huyo kutoka eneo la North Rift ambaye aliomba tulibane jina lake akidai yeye sio msemeja wa UDA.

Haya yanajiri wakati ambapo UDA imezongwa na mivutano miongoni mwa nyota wake katika kaunti za Nakuru na Uasin Gishu wanaong’ang’ania udhibiti wa matawi ya chama hicho.

Katika kaunti ya Nakuru mrengo mmoja unaoongozwa na Seneta Susan Kihika na mwingine unaoongozwa na Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri inang’ang’ania udhibiti wa UDA katika kaunti hiyo.

Haswa wanasiasa hao wametofautiana kuhusu uteuzi wa mshirikishi wa chama hicho katika kaunti hiyo. Mrengo wa Bi Kihika unataka wadhifa huo umwendee aliyekuwa mgombeaji wa ubunge wa Rongai katika uchaguzi mkuu wa 2017 Paul Chebor. Lakini mrengo wa Bw Ngunjiri unataka wadhifa huo umwendee bintiye Ngunjiri, Edith Kimani.

Kwa mara nyingine katika kaunti ya Uasin Gishu, tofauti zimeibuka baina ya Mbunge wa Soy Caleb Kositany na mwenzake wa Kapseret Oscar Sudi kuhusu suala lilo hilo la uteuzi wa mshiriki wa UDA katika kaunti.

Huku Bw Kositany akimpendekeza mwandani wake kwa jina Joseph Kiprop Bw Sudi anapinga wazo hilo akisema wanachama UDA tawi la Uasin Gishu ndio wanafaa kupewa nafasi ya kuchagua yule ambaye wanahisi kuwa atafaa kwa wadhifa huo muhimu.

“Nafasi muhimu kama hii haifaa kushikiliwa na mtu ambaye ni kibaraka cha mwanasiasa fulani ambaye anataka kuendeleza ajenda zake za kibinafsi kupitia chama cha UDA. Tawi la Uasin Gishu ni muhimu zaidi kwa sababu ndiko anakotoka mgombeaji wetu wa urais na hivyo sharti liongozwe na mtu mwenye maono na ambaye ataendeleza chama kwa weledi mkubwa,” Bw Sudi anasema.

Lakini alitoa hakikisho kuwa mwafaka utapatikana kwa lengo la kukiwezesha chama hicho kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2022.

Kuhusu mzozo wa Nakuru, Bw Kimani pia anamshikilia kuwa tofauti kati yake na Seneta Kihika hazitayumbisha uthabiti wa UDA katika kaunti hiyo.

“UDA ni thabiti zaidi katika kaunti ya Nakuru. Ni hii ilidhihirishwa kupitia ushindi wa Bw Anthony Nzuki Wachira katika uchaguzi mdogo wa wadi ya London. Shida ndogo ndogo ibuka zitashughulikiwa hivi karibuni,” akaambia Taifa Jumapili.

“Nawataka wanachama kuwa watulivu. Tulitangazwa kuwa kutakuwepo wa washirikishi wa UDA katika kila ngazi za Kaunti, eneo bunge na wadi, watu wengine walielewa vibaya. Walidhani ni mwanya ya wao kudhibiti chama kwa manufaa yao ya kibinafsi,” Bw Kimani anaongeza.

Hayo yanajiri huku duru zikisema kuwa mvutano kati ya mbunge huyo na Seneta Kihika unasababisha mgawanyiko mkubwa miongoni mwa wanachama wa UDA katika kaunti ya Nakuru.

Duru ziliambia Taifa Jumapili kwamba tofauti sawa na hizo zimeshamiri katika kaunti ya Nandi kati ya mirengo ya Gavana Stephen Sang na Seneta Samson Cherargei. Kila mmoja anataka kuweka kibarakaka chake kuwa shirikishi wa UDA katika kaunti hiyo

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa James Mwamu anasema kuwa Dkt Ruto anafaa kuzima tofauti hizi ili aweze kufaulu kuifanya UDA kuwa thabiti kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

“Dalili kwamba wabunge kutoka eneo la magharibi mwa Kenya kama vile Didmus Barasa na John Waluke wameanza kujiondoa kutoka vuguvugu la Hasla pia ni changamoto nyingine katika juhudi za kukiimarisha UDA katika eneo hilo lenya idadi kubwa ya kura,” akasema.

Kando na hayo katika siku za hivi karibuni wandani wa Dkt Ruto kutoka eneo la Mlima Kenya na Pwani hawajakuwa wakionyesha kujitolea kwao katika kuvumisha chama cha UDA katika maeneo yao.

Huku baadhi ya wandani wake kutoka Pwani kama vile Aisha Jumwa (Mbunge wa Malindi) na mwenzake wa Kilifi Kaskazini Owen Baya wakichangamkia wazo la kubuni kwa chama mahsusi cha Pwani, wenzao wa Mlima Kenya nao wamekuwa wakijihusisha na vyama vidogo.

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria anaendelea kuvumisha chama chake cha People’s Empowerment Party (PEP) huku wanasiasa wengine wakiaza kujivumisha chama The Service Party chake Waziri wa zamani wa Kilimo Moses Kuria.

Hata hivyo, Dkt Ruto anashikilia kuwa UDA ndicho chama atakachotumia katika uchaguzi wa urais mwaka ujao.

Kwenye mahojiano na Redio Citizen mnamo Alhamisi Dkt Ruto aliweka wazi kwamba analenga kukiimarisha chama cha UDA na kuhakikisha kuwa kinapata sura ya kitaifa “kwani ndicho chombo ambacho nitatumia kufanikisha safari yangu ya Ikulu kwani Jubilee imetekwa na matapeli.”

“Chama cha UDA na kile Jubilee ni mamoja, kwa sababu vilitia saini mkataba wa ushirikiano. Hii ndio maana naona UDA chama chombo mbadala ambacho nitakutumia kuendeleza sera ambazo tulikuwa nazo tulipobuni Jubilee 2016,” akasema.

Kwa hivyo, kulingana na Bw Mwamu, Dkt Ruto hana budi kuzima misukosuko inayotokota ndani ya UDA ili aweze kufikia lengo hili.

You can share this post!

Mahangaiko aliyopitia hayakuzima ndoto zake kuwa msanii,...

Faida za lozi