• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:55 AM
Je, Raila ni mwanamageuzi au kiongozi mbinafsi?

Je, Raila ni mwanamageuzi au kiongozi mbinafsi?

WANDERI KAMAU Na RUSHDIE OUDIA

MASWALI yameibuka kuhusu kinachompa kiongozi wa Azimio la Umoja, Raila Odinga, mshawasha wa kuendelea na harakati wa kupigania kile anachokitaja kuwa haki na usawa katika jamii.

Wengi wanashangaa anakotoa nguvu na msukumo katika juhudi zake za kushinikiza mageuzi ya kisiasa. Na kwenye safari hii ndefu ya kupigania utawala unaozingatia demokrasia, mara nyingi hutofautiana na washirika wake au hata juhudi zake hukosa kufaulu kama alivyopanga, na kwa hayo yote huwa hatamauki.

Anapojitayarisha kuwaongoza wafuasi wake kwa maandamano makubwa dhidi ya serikali ya Rais William Ruto Jumatatu ijayo, hii haitakuwa mara ya kwanza kwa Bw Odinga kuwakabili wapinzani wake kwa ‘kumnyang’anya ushindi.’

Bw Odinga anasisitiza kuwa Rais Ruto hakushinda kihalali kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, licha ya kutangazwa mshindi na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na baadaye kuidhinishwa na Mahakama ya Upeo.

Mnamo 1998, Bw Odinga alibuni ushirikiano wa kisiasa na Rais Mstaafu (marehemu) Daniel Moi, baada ya kuunganisha chama chake cha National Development Party (NDP) na Kanu kuunda chama cha New-Kanu.

Mnamo Juni 2001, Bw Odinga aliteuliwa kuwa Waziri wa Kawi na baadaye Katibu Mkuu wa New-Kanu kufuatia muungano huo.

Washirika wake kadhaa katika NDP na eneo la Luo Nyanza pia waliteuliwa kuwa mawaziri na mawaziri wasaidizi na Moi.
Hata hivyo, ‘urafiki’ baina ya Raila na Moi ulikatika miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa 2002, baada ya Moi kumtangaza Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kama mwaniaji urais wa Kanu.

Kwa kuhisi kusalitiwa na Moi, Bw Odinga aliwaongoza washirika wake kujiondoa katika Kanu na kubuni chama cha Liberal Democratic Party (LDP). Miongoni mwa wanasiasa alioondoka pamoja nao ni marehemu George Saitoti, William Ole Ntimama kati ya wengine.

Bw Odinga aliungana na Rais Mstaafu (marehemu) Mwai Kibaki ambapo walibuni muungano wa NARC, uliowawezesha kuibuka washindi kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2002. Ingawa muungano huo ulionekana kuwapa matumaini Wakenya wengi, tofauti ziliibuka tena baina ya Bw Kibaki na Bw Odinga.

Bw Odinga na washirika wake walimlaumu Bw Kibaki kwa kukiuka Mkataba wa Makubaliano (MoU) ulioeleza kuwa Bw Kibaki alifaa kumteua Bw Odinga Waziri Mkuu mwenye mamlaka baada yao kuifanyia mageuzi katiba.

Mnamo 2005, Bw Odinga aliongoza kampeni za kupinga Katiba, ambapo mrengo wake uliibuka mshindi dhidi ya serikali ya Rais Kibaki. Hilo lilimfanya Bw Kibaki kumfuta kazi pamoja na mawaziri wengine waliopinga Katiba.

Mnamo 2007, Bw Odinga alikataa kukubali matokeo ya urais yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi Kenya (ECK), ambapo Bw Kibaki aliibuka mshindi.

Kutokana na ghasia zilizoibuka baada ya uchaguzi huo tata, ilimlazimu Bw Kibaki na Bw Odinga kubuni Serikali ya Muungano wa Kitaifa, ambapo Bw Odinga alihudumu kama Waziri Mkuu.

Juhudi za kuwapatanisha viongozi hao wawili ziliongozwa na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa (UN) marehemu Kofi Annan.

Kwa mara nyingine, ilimlazimu Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kufanya handisheki na Bw Odinga, baada ya (Odinga) kudai kuwa uchaguzi mkuu wa 2017 ulikumbwa na udanganyifu.

Hii ni baada ya Mahakama ya Upeo kufutilia mbali uchaguzi wa urais, kufuatia kesi iliyowasilishwa na muungano wa Nasa, wake Bw Odinga. Bw Kenyatta alikuwa ametangazwa kuwa mshindi na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC). Bw Odinga alikataa kushiriki kwenye duru ya pili ya uchaguzi huo, akidai hakuwa na imani na utendakazi wa IEBC.

Kwa sasa, Rais Ruto anajipata kwenye njiapanda kama watangulizi wake, kufuatia tishio la maandamano ambalo limetolewa na kiongozi huyo.

Jana Jumatano jijini Kisumu, iliwalazimu polisi kuwakabili wafuasi wa Bw Odinga baada yao kutishia kuvamia Ikulu Ndogo ya Kisumu.

Kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo’, baadhi yao walisema “wanafanya mazoezi” wanapojitayarisha kwa maandamano makubwa Jumatatu, baada ya Bw Odinga kuitangaza kuwa siku ya mapumziko.
Kufuatia mwelekeo huo, wadadisi wanautaja msukumo wa Bw Odinga kujengwa na safari ngumu ya kisiasa ambayo amepitia.

Kwenye mahojiano Jumatano, mdadisi wa siasa Javas Bigambo alisema juhudi za mwanasiasa huyo zinatokana na mazingira magumu ya kisiasa aliyokulia.

“Bw Odinga si mwanasiasa wa jana. Yeye si mwanasiasa wa kizazi hiki, bali ni mtu aliyeanza uanaharakati wake akiwa mchanga sana, katika miaka ya 1970 na 1980. Aliukabili utawala wa Moi, kiasi cha kufungwa gerezani kwa miaka tisa,” akasema Bw Bigambo.

Anasema Bw Odinga alipaliliwa kisiasa na wanasiasa wenye msimamo mkali kama vile babake, marehemu Jaramogi Oginga Odinga, Kenneth Matiba, Masinde Muliro, George Anyona kati ya wengine.

“Kizazi cha akina Jaramogi ndicho kilimshinikiza Moi kubadilisha sehemu 2 (a) ya Katiba na kuruhusu uwepo wa vyama vingi vya kisiasa nchini. Ushindi ambao kizazi hicho kilipata dhidi ya Moi ndio unaoonekana kumsukuma Bw Odinga,” akasema.

Anaeleza kuwa kupitia misukumo hiyo, lengo jingine la Bw Odinga ni kukijenga kizazi kingine cha wanasiasa kitakachofuata nyayo za watangulizi wake.

  • Tags

You can share this post!

NEMA yataka mahakama itupe kesi inayopinga usafirishaji wa...

Gavana Nassir aonya mawaziri wake dhidi ya uzembe

T L