• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Jinsi walivyojifunga jela kwa kuabiri basi la Azimio

Jinsi walivyojifunga jela kwa kuabiri basi la Azimio

NA LEONARD ONYANGO

KUSHINDWA kwa Gavana wa Kilifi Amason Kingi na mwenzake wa Machakos Dkt Alfred Mutua kuondoa vyama vyao kutoka Azimio la Umoja One Kenya kumefanya vyama tanzu 25 kung’amua jinsi vilivyojifunga katika muungano huo.

Kulingana na Msajili wa Vyama vya Kisiasa chama cha Pamoja African Alliance (PAA) chake Gavana Kingi na Maendeleo Chap Chap vimefungiwa ndani ya Azimio hadi Machi 2023 sawa na vingine 24.

Vyama hivyo viliingia ndani ya Azimio kupitia chama cha Jubilee kinachoongozwa na Rais Kenyatta.

Chama cha PAA kilitia saini mkataba wa maelewano na Jubilee Februari 25, 2022.

Kupitia mkataba huo, masilahi ya PAA yanafaa kutetewa na Rais Kenyatta ndani ya serikali ya Azimio iwapo mwaniaji wake wa urais, Raila Odinga, ataibuka mshindi katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Hali hii ndio pia inakumba vyama vingine zaidi ya 20 vilivyoingia Azimio kupitia Jubilee, ambayo ni mshirika mkuu katika muungano huo pamoja na chama cha ODM chake Raila Odinga.

Bw Odinga ndiye mwaniaji urais wa Azimio la Umoja One Kenya na baadhi ya vyama vinalalamikia uteuzi wa mwaniaji mwenza wake.

Hii ni miongoni mwa masuala ambayo yamekera baadhi ya vyama tanzu kiasi cha kujaribu kujiondoa katika Azimio.

Wiki iliyopita Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Bi Anne Nderitu, alikataa kuruhusu vyama vya PAA na MCC kujiondoa Azimio.

Alisema kuwa mkataba wa maelewano umepiga marufuku vyama kujiondoa katika muungano huo miezi sita kabla na miezi mitatu baada ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Chama kinachotaka kujiondoa pia kitatoa notisi ya miezi mitatu. Hiyo inamaanisha kuwa vyama vilivyo ndani ya Azimio haviwezi kuondoka kati ya Aprili mwaka huu na Machi 2023.

Japo Gavana Kingi anadai kuwa ametengwa katika kampeni za Azimio haswa eneo la Pwani, kujumuishwa kwa Gavana Hassan Joho wa Mombasa katika Baraza Kuu la Azimio pia kunaonekana kumkera.

Kulingana na duru ndani ya PAA, Gavana Kingi anahofia kuwa hatua hiyo itampa Bw Joho nafasi nzuri ya kupata uwaziri ndani ya serikali ya Azimio.

“Wengi wanategea uwaziri katika serikali ya Azimio, itakuwa vigumu kwa watu wawili kutoka eneo la Pwani kuteuliwa mawaziri,” akasema afisa wa chama cha PAA aliyeomba jina libanwe.

Chama cha Wiper kupitia uliokuwa muungano wa One Kenya Alliance (OKA) kiliandika barua ya kutaka mkataba wa Azimio kusitishwa kwa muda, baada ya kuibuka kwa ripoti kwamba Bw Odinga anapendelea magavana wa kaunti tatu za Ukambani.

Magavana hao Charity Ngilu (Kitui), Alfred Mutua (Machakos) na Kivutha Kibwana (Makueni) nao wanahisi kwamba kuwepo kwa Musyoka katika Azimio kunazima nyota yao.

Hii ndiyo sababu ya Dkt Mutua kujaribu kujiondoa katika muungano huo kabla ya juhudi hizo kugonga mwamba.

  • Tags

You can share this post!

Kura ya maoni yamweka Raila mbele ya Ruto jijini Nairobi

TAHARIRI: Wanafunzi wasinyimwe masomo kwa sababu ya karo

T L