• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 1:14 PM
TAHARIRI: Wanafunzi wasinyimwe masomo kwa sababu ya karo

TAHARIRI: Wanafunzi wasinyimwe masomo kwa sababu ya karo

NA MHARIRI

KUANZIA leo, wazazi watakuwa wakipeleka watoto wao waliofanya mtihani wa Darasa la Nane kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za sekondari.

Hii ni siku 12 tu baada ya matokeo kutangazwa na wengi wamelalamikia ugumu wa kupata karo kutokana na hali mbaya ya uchumi wa nchi.

Huu ni ukweli ambao kila mdau katika sekta ya elimu anakubaliana nao.

Hivyo basi, kuna haja ya walimu wakuu wa shule kuwasikiliza wazazi ambao huenda wakakosa karo yote inayohitajika watoto wao wasajiliwe katika Kidato cha Kwanza.

Ni kweli kuwa, walimu wakuu wanakabiliwa na wakati mgumu kuendesha shule hasa za mabweni.

Hata hivyo, kuna mahitaji yasiyo na umuhimu kunyima mwanafunzi nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza kufanikisha ndoto yake.Kama alivyosema Waziri wa Elimu Profesa George Magoha wiki chache zilizopita, walimu wakuu wanapaswa kuwa na utu na kuwasikiliza wazazi ambao hawatapata karo yote kwa sababu wasizoweza kuepuka.

Kumekuwa na ripoti za baadhi ya walimu wakuu kuwa katili kiasi cha kuwafukuza wazazi na watoto wao wakifika shuleni bila karo yote inayohitajika.

Tabia hii haifai kuruhusiwa kwa kuwa ni pigo kwa juhudi za serikali za kuhakikisha watoto wote wanaofanya mtihani wa darasa la nane wanajiunga na shule ya sekondari.

Huu ni ubaguzi usioruhusiwa kikatiba kwa kuwa unanyima mtoto haki yake ya elimu kwa sababu ambazo hawezi kuzidhibiti.

Walimu wakuu, kama wadau katika sekta ya elimu, wanafaa kuwa kwenye msitari wa mbele kuhimiza watoto kusoma.

Serikali nayo inapaswa kutekeleza jukumu lake kwa kuadhibu walimu wakuu wanaokosa kuheshimu haki ya watoto ya kusoma kwa kukataa kuwasajili kujiunga na kidato cha kwanza na pia wale wazazi wao wanachelewa kulipa karo.

Hii haimaanishi wazazi walegeze juhudi za kulipa karo kwa kuwa walimu pia wanakabiliwa na wakati mgumu kukidhi mahitaji muhimu shuleni.

Kuna wazazi waliojaliwa mapato ya juu na hivyo hawajaathirika pakubwa kutokana na hali ngumu ya kiuchumi inayoendelea kwa wakati huu.

Wazazi kama hao wasisubiri kupata afueni kutoka kwa wasimamizi wa shuleSerikali pia iwajibike kwa kutoa pesa za kufadhili elimu bila malipo kwa wakati ufaao.

You can share this post!

Jinsi walivyojifunga jela kwa kuabiri basi la Azimio

Mbunge akosoa vikali hatua ya chama kwa kujiunga na Ruto

T L