• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 5:56 PM
Jubilee pazuri kutwaa ugavana Nairobi

Jubilee pazuri kutwaa ugavana Nairobi

Na LEONARD ONYANGO

CHAMA cha Jubilee kimewaidhinisha wandani wa Rais Uhuru Kenyatta kupigania tiketi ya chama hicho kuwania ugavana Nairobi katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Februari 18, 2021.

Jubilee Jumatatu iliidhinisha aliyekuwa mbunge wa Dagoretti Kusini Denis Waweru (pichani) na mfanyabiashara Agnes Kagure kupigania uteuzi wa chama hicho kwenye mchujo.

Nacho chama cha ODM kiliidhinisha mwenyekiti wa vuguvugu la wanawake wa ODM, Beth Syengo na aliyekuwa naibu mkurugenzi wa Idara ya Ujasusi (NIS), Sam Wakiaga kushiriki kura za mchujo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Uchaguzi ya ODM, Catherine Mumma jana aliambia Taifa Leo kuwa ni wawili hao tu ambao walituma maombi ya kutaka kuwania ugavana wa Nairobi.

Kiti hicho kilibaki wazi baada ya Mike Sonko kung’olewa awali mwezi huu.Vyama vya Jubilee na ODM vilikuwa vimewataka waliotaka kuwania ugavana kupitia tiketi ya vyama hivyo kuwasilisha maombi yao kufikia jana saa sita mchana.

Iwapo hakutakuwa na maafikiano miongoni mwa wawaniaji, vyama vya Jubilee na ODM vitatakiwa kuandaa kura za mchujo kabla ya Januari 19.Bw Waweru ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa ofisi ya Mpango wa Maridhiano (BBI) na Bi Kagure, wote ni wandani wa Rais Kenyatta.

Wadadisi wa masuala ya siasa wanasema kuwa iwapo Naibu Rais William Ruto atapigia debe mwaniaji tofauti na wa Jubilee, huenda mahasimu wake wa kisiasa wakaanzisha shinikizo za kumtaka ajiuzulu kwa kukiuka itikadi ya chama. Duru za kuaminika zilidokezea Taifa Leo kuwa huenda chama cha ODM kikaunga mkono mwaniaji wa Jubilee.

“Jubilee watatoa gavana na sisi naibu gavana,” akasema mmoja wa viongozi wa ngazi ya juu katika ODM aliyeomba jina lake libanwe.Kwa mujibu wa ratiba ya IEBC, vyama vya kisiasa vinastahili kusuluhisha mizozo inayotokana na uteuzi au kura za mchujo kufikia Januari 11.

IEBC itapokea majina ya watakaoteuliwa na vyama kati ya Januari 18 na Januari 19.

You can share this post!

Huzuni tele viongozi wakipoteza wazazi wao

Daktari akana kunyemelea na kubaka mwanafunzi