• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Kakaye Joho aongoza waliokosa tikiti kuhama UDA

Kakaye Joho aongoza waliokosa tikiti kuhama UDA

NA WINNIE ATIENO

KAKA wa Gavana wa Mombasa Hassan Joho, ambaye alikuwa akiwania kiti cha useneta katika Kaunti ya Mombasa kupitia chama cha United Democratic Alliance (UDA) chake Naibu Rais William Ruto ameongoza wawaniaji waliokosa tikiti kuhama chama hicho.

Bw Mohammed Amir ambaye alihama ODM na kujiunga na United Democratic Alliance (UDA) kugombea useneta, alifichua masaibu waliyokumbana nayo kabla ya mchujo wa chama hicho.

Wawaniaji hao wamedai kwamba walibanduliwa kwenye mchujo na wakuu wa chama hicho.

“Mchujo wa chama haukuwa huru wala wa usawa, hapakuwa na haki hata kidogo. Kulikuwa na upendeleo hasa hapa Mombasa; kuna baadhi ya viongozi wa chama ambao

walinibagua sababu ya ukoo na familia yangu. Mnachosahau ni kwamba licha ya ukoo, ndugu huwa hawafanani,” alisema Bw Amir.

“Nilidhania kungekuwua na usawa na haki lakini kumbe kuna watu waliokuwa na ajenda zao za kibinafsi na walikuwa wanataka kulipiza kisasa kwangu wakaamua kuniangusha. Nimeamua kusimama kama mgombea huru,” akamsemeza Naibu wa Rais, Dkt William Ruto.

Mwenyekiti wa wawaniaji wa udiwani katika chama cha UDA Mombasa, Bw Aziz Mbuzi alisema mchujo ulikuwa na dosari nyingi.

“Ninagombea kiti cha Ziwa la Ng’ombe lakini mchujo ulikuwa wa maajabu, majina yalikosekana katika sajili. Nani anagawa uongozi Mombasa? UDA Mombasa itakosa viti vingi sana sababu wagombeaji na wafuasi wao wamekasirika. Tunataka haki,” alisema.

Bw Ibrahim Dube ambaye alikuwa anawania kiti cha Tononoka alisema sajili ya chama haikuwa na jina lake.

“Hata wafuasi wangu walikosekana ilhali mpinzani wangu alitangazwa mshindi. Tumetumia pesa, mali na muda wetu kwa chama lakini mwishowe tunatupwa nje. Mungu yuko,” alisema.

Mgombeaji wa kiti cha ene – obunge la Mvita, Bw Hassan Rajab Sumba alisema mpinzani wake Omar Shallo alipendelewa na chama ndiposa akapewa tikiti.

“Tumefanyiwa unyonge wa hali ya juu. Hii si usawa ila ni dhuluma, kwa nini Bw Shallo apewe tikiti? Kwa nini hatukuenda mchujo?” aliuliza. Alisema bado yuko kwenye kinyang’ayiro.

Hata hivyo, mgombeaji wa ugavana kupitia UDA, Bw Hassan Omar alisema Bw Ruto hakutoa tikiti ya moja kwa moja kwa wagombeaji bali ilikuwa ni kupitia maelewano.

Wafanyabiashara wa Kongowea ambao wanampigia debe Bw Ahmed Siyat, mwaniaji wa wadi ya Kongowea, waliandamana wakipinga mchujo wa chama cha UDA.

Walisema Bw Siyat alinyimwa haki na kuapa kuhama chama hicho na kutomuunga mkono Dkt Ruto.

  • Tags

You can share this post!

Nassir amshukuru Shahbal kwa kumwachia nafasi ya ugavana

Uhuru atakavyodhibiti serikali ya Raila

T L