• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Nassir amshukuru Shahbal kwa kumwachia nafasi ya ugavana

Nassir amshukuru Shahbal kwa kumwachia nafasi ya ugavana

NA WINNIE ATIENO

MWANIAJI wa ugavana wa Mombasa kwa tikiti ya ODM, Bw Abdulswamad Nassir amemshukuru mfanyabiashara Suleiman Shahbal kwa kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha kumrithi Gavana Hassan Joho.

Bw Nassir pia amemuomba Bw Shahbal kushirikiana naye ili ODM ipate ushindi na kutimiza ahadi zao na matarajio kwa wakazi wa Mombasa.

Wawili hao ambao walikuwa mahasimu wa kisiasa walikuwa wakimenyania tikiti ya ODM.

Hata hivyo, kinara wa chama cha ODM, Raila Odinga alimchagua Bw Nassir kupeperusha bendera ya chama.

“Nimekubali uteuzi wa chama kwa unyenyekevu mkubwa kugombea ugavana wa Mombasa katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9. Nitapeperusha bendera ya chama chetu cha ODM katika Kaunti

ya Mombasa. Ni heshima kubwa kupewa jukumu hili na ninatoa ahadi yangu kwamba nitatimiza malengo yetu,” akasema Bw Nassir.

Alimshukuru Bw Odinga na wananchi wa Mombasa kwa kuwa na imani naye.

“Na pia kwa kaka yangu Bw Shahbal kwa kuweka kando azma yake ya ugavana na kuniunga mkono; Mombasa imeungana. Kwa kakangu Hassan Joho, ambaye pia ni naibu kiongozi wa chama, ninanuia kuendeleza sekta nyingi ambazo zimeimarika chini ya uongozi wako,” alisema.

Bw Nassir alisema ananuia kujifunza kutokana na changamoto ambazo serikali ya Bw Joho ilikumbana nazo ili kuimarisha Mombasa.

“Kwa wananchi wenzangu wa Mombasa, hii itakuwa safari yetu sote. Mungu akipenda hatutashindwa,” alisema.

Viongozi wenzake wakiongozwa na wabunge Mishi Mboko (Likoni) na Badi Twalib (Jomvu) pia walimpongeza kwa kupata tikiti.

Bw Sahbal ambaye ameshirikishwa katika ofi – si ya kitaifa ya kampeni za Bw Odinga alisema ataendelea kumpigia debe waziri mkuu huyo wa zamani ili ashinde urais.

“Nimekuwa nikigombea ugavana wa Mombasa kwa miaka 10 iliyopita, lakini nia haikuwa ni ya Shahbal bali kuleta maendeleo na mabadiliko kwa wakazi wa Mombasa. Lakini si lazima Shahbal ndiye alete mabadiliko hayo Mombasa; muhimu ni kuwa mabadiliko hayo yaletwe,” akasema Bw Shahbal.

Alisema baada ya kutafakari sana pamoja na mazungumzo marefu na Bw Odinga na ushauri kutoka kwa mwenyekiti wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Rais Uhuru Kenyatta, aliamua kumuunga mkono Bw Nassir.

  • Tags

You can share this post!

Washirika wa Ruto wadai Uhuru na Raila wamemsaliti Kalonzo

Kakaye Joho aongoza waliokosa tikiti kuhama UDA

T L