• Nairobi
  • Last Updated December 4th, 2023 8:09 PM
Uhuru atakavyodhibiti serikali ya Raila

Uhuru atakavyodhibiti serikali ya Raila

NA LEONARD ONYANGO

RAIS Uhuru Kenyatta atakuwa na usemi mkubwa katika serikali ya muungano wa Azimio iwapo mwaniaji wake Raila Odinga atashinda urais katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, imebainika.

Kulingana na taarifa iliyochap – ishwa Alhamisi katika Gazeti Rasmi la Serikali, Rais Kenyatta atakuwa mwenyekiti wa Baraza Kuu la Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.

Bw Odinga atakuwa kiongozi wa muungano wa Azimio huku Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya, kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa Kanu Gideon Moi, Gavana wa Mombasa Hassan Joho, mbunge wa Murang’a Sabina Chege na mbunge wa Taita Taveta Naomi Shaban wakiwa wajumbe wa baraza hilo.

Wajumbe wengine watakuwa kiongozi wa NARC Kenya, Martha Karua, Gavana wa Kitui Charity Ngilu, Abdi Noor Omar Farah na kiongozi wa chama cha Democratic Action Party – Kenya (DAP-K) Wafula Wamunyinyi.

Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed atakuwa Katibu Mkuu wa Baraza hilo.

Kulingana na katiba ya muungano wa Azimio iliyohifadhiwa katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa Ann

Nderitu, wajumbe wa Baraza Kuu la Azimio watakutana angalau mara moja baada ya miezi mitatu.

Mwenyekiti ambaye ni Rais Kenyatta ndiye ametwikwa mamlaka ya kuitisha kikao cha baraza hilo wakati wowote.

“Wajumbe wa Baraza Kuu watakutana angalau mara moja baada ya miezi mitatu au wakati wowote kulingana na maelekezo ya mwenyekiti,” inasema Katiba hiyo iliyotazamwa na mwandishi wetu.

Baada ya Uchaguzi Mkuu, wabunge wa vyama 26 vilivyo ndani ya muungano wa Azimio, wataunda vuguvugu ambalo pia litajumuisha wabunge maalumu na wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Jukumu la vuguvugu hilo litakuwa kutetea sera za serikali ya Azimio bungeni.

Hata hivyo, Rais Kenyatta atakuwa na usemi mkubwa katika uteuzi wa kiongozi wa vuguvugu hilo la wabunge.

Iwapo kutakuwa na jambo lenye utata ambalo litagawanya wajumbe wa Baraza Kuu la Azimio, Uhuru ambaye atakuwa Rais Mstaafu wakati huo atapiga kura ya kuamua.

Rais Kenyatta pia atakuwa na usemi katika uteuzi wa wajumbe wa Kamati ya Nidhamu ambayo itapambana na wabunge wa Azimio wanaokiuka maadili kwa kuendeleza ajenda za mrengo wa upinzani.

Baraza Kuu ambalo mwenyekiti

wake ni Rais Kenyatta pia linaweza kutambua wabunge wakorofi na kua – giza kamati ya Nidhamu kuwashughulikia.

Kamati ya Nidhamu imepewa mamlaka ya kutoza faini, kutimua chamani au kuondoa mbunge kutoka kwenye kamati za Bunge.

Katiba ya Azimio imempa Rais Kenyatta na Bw Odinga mamlaka ya kufanya maamuzi kwa niaba ya muungano wa Azimio hadi pale Baraza Kuu litakapoanza vikao vyake.

“Kabla ya Baraza Kuu kuanza rasmi vikao vyake, maamuzi yatakayofanywa na kiongozi wa Jubilee (Rais Kenyatta) na kiongozi wa ODM (Bw Odinga) yatachukuliwa kuwa maamuzi ya baraza,” inasema katiba ambayo imepiga marufuku vyama wanachama kujiondoa miezi sita kabla ya Uchaguzi Mkuu na miezi mitatu baadaye.

Baraza Kuu limetwikwa majukumu ya kuongoza muungano wa Azimio na ndilo litatoa mwelekeo unaofaa kuchukuliwa na vyama wanachama.

Baraza pia limekubaliwa kusajili vyama vinavyohitaji kujiunga na muungano wa Azimio baada ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Chama cha Jubilee kimeingia maelewano na zaidi ya vyama 10 ambavyo Rais Kenyatta atashughulikia maslahi yavyo ndani ya muungano wa Azimio.

Hiyo inamaanisha kuwa upande wa Rais Kenyatta huenda ukawa na wabunge wengi zaidi ikilinganishwa na vyama vingine ndani ya muungano, hivyo kuwa na usemi mkubwa.

Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni anasema kuwa chama hicho pia kitatoa mwaniaji mwenza wa Bw Odinga katika juhudi za kutaka kuwa na usemi zaidi katika serikali ijayo.

Mrengo wa Naibu wa Rais William Ruto, hata hivyo, umekosoa hatua ya Rais Kenyatta kuteuliwa mwenyekiti wa Baraza Kuu la Azimio huku ukidai kuwa hiyo ni ishara kwamba kiongozi wa nchi hana mpango wa kustaafu kutoka kwenye siasa baada ya kukamilisha muhula wake baada ya Uchaguzi Mkuu ujao.

Wazee wa jamii ya Wakikuyu mwezi uliopita walimuongezea Rais Kenyatta miaka mitano zaidi ya kuongoza jamii hiyo.

Chama cha Jubilee pia kilimteua Rais Kenyatta kuendelea kuwa kiongozi wake hata baada ya kustaafu.

  • Tags

You can share this post!

Kakaye Joho aongoza waliokosa tikiti kuhama UDA

Mivutano Azimio inavyohujumu mipango ya Raila kuingia Ikulu

T L