• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Kalonzo ajitokeza hadharani baada ya kutoonekana wakati wa maandamano

Kalonzo ajitokeza hadharani baada ya kutoonekana wakati wa maandamano

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka mnamo Jumamosi alionekana wazi tangu Jumanne baada ya uvumi kuenea kuwa alizuiwa nyumbani kwake na maafisa wa usalama asitoke kwenda kuongoza maandamano dhidi ya serikali.

Bw Musyoka alijitokeza katika afisi za SKM Centre mtaani Karen alikoungana na viongozi wengine wa Azimio kuwahutubia wanahabari.

Miongoni mwa viongozi hao walikuwa ni; Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni, Kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa, Gavana wa zamani wa Murang’a Mwangi Wa Irian na kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa Opiyo Wandayi.

Aidha, Bw Musyoka alitumia fursa hiyo kuthibitisha kuwa alikutana na mabalozi wa mataifa ya Amerika, Uingereza na Uholanzi mnamo Ijumaa nyumbani kwake, Karen Nairobi.

“Mabalozi wa Amerika, Uingereza na Uholanzi na Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa walikuja nyumbani kwangu na tukashauriana. Hata hivyo, tuliafikiana kuwa hatungeongea na wanahabari,” akaeleza.

“Walielezea kughadhabishwa kwao kwamba maandamano ya amani yaligeuzwa na polisi na kuwa uwanja wa fujo na maafa,” Bw Musyoka akasema.

Kiongozi huyo wa Wiper alisema kinara wa Azimio Raila Odinga, kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua na Naibu Kiongozi wa ODM Wycliffe Oparanya hawangeweza kuhudhuria mkutano huo kwa sababu walikuwa wamebanwa na shughuli nyingine kwingineko.

Bw Musyoka aliongeza kuwa makazi ya kiongozi wa chama cha Roots George Wajackoyah yaliyoko magharibi mwa Kenya yalivamiwa na watu walioaminika kuwa maafisa wa usalama.

Kiongozi wa chama cha Usawa kwa Wote Bw Mwangi Wa Iria alisema kuwa Azimio haitafanya mazungumzo na Kenya Kwanza kwa sababu iliamuru kupigwa risasi kwa waandamanaji wasio na silaha.

Bw Wa Iria ambaye pia ni gavana wa zamani wa Murang’a alitangaza kuwa maandamano ya Azimio yatarejelewa Jumatano wiki ijayo.

“Tutatoa notisi kwa maafisa wasimamizi wa vituo vya polisi (OCS) kote nchini ili watume polisi wa kutoa usalama kwa waandamanaji,” akasema Bw Wa Iria.

Viongozi hao waliitaka serikali kuamuru kuachiliwa huru kwa wabunge na wafuasi wa Azimio ambao bado wanazuiliwa baada ya kukamatwa kuhusiana na maandamano ya wiki hii.

  • Tags

You can share this post!

Omanyala apata windo alilotafuta mjini Monaco

Sukari: Kamati yaambiwa wabunge 2 walipelelezwa na DCI

T L