• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:01 AM
Omanyala apata windo alilotafuta mjini Monaco

Omanyala apata windo alilotafuta mjini Monaco

NYOTA Ferdinand Omanyala na Faith Kipyegon waliendelea kupatia Kenya matumaini ya kupata medali kwenye Riadha za Dunia nchini Hungary baada ya kutawala mbio za mita 100 na maili moja wakati wa Monaco Diamond League Ijumaa, mtawalia.

Bingwa wa Afrika na Jumuiya ya Madola 100m Omanyala aliandikisha ushindi wake wa kwanza kabisa kwenye Diamond League alipotetemesha Monaco kwa sekunde 9.92.

Mshikilizi huyo wa rekodi ya Afrika ya 9.77 alimaliza mbele ya Mbotswana Letsile Tebogo (9.93) na Ackeem Blake kutoka Jamaica (10.00).

Samuel Koech (3000m kuruka viunzi na maji) na Wycliffe Kinyamal (800m) pia walinyakua mataji ya vitengo vyao katika siku ambayo Mary Moraa alionyeshwa kivumbi katika 400m.

Kipyegon alifyatuka maili moja kwa rekodi ya dunia ya dakika 4:07.64. Alifuta rekodi ya Mholanzi Sifan Hassan ya 4:12.33 iliyokuwa imara tangu 2019.

Bingwa huyo mara mbili wa Olimpiki na dunia wa 1500m alifuatiwa na Ciara Mageean aliyeweka rekodi ya kitaifa ya Ireland (4:14.58) na Muethiopia Freweyni Hailu (4:14.79).

Kipyegon atawakilisha Kenya katika vitengo vya 1500m na 5000m kwenye Riadha za Dunia mjini Budapest mnamo Agosti 19-26.

Anashikilia rekodi tatu sasa za dunia. Alifuta ya 5000m ya Letesenbet Gidey ya dakika 14:06.62 na ya 1500m ya Genzebe Dibaba ya 3:50.07 akishinda vitengo hivyo kwa 14:05.20 na 3:49.11 kwenye Diamond League mwezi Juni nchini Italia na Ufaransa, mtawalia.

“Ni baraka kupata rekodi ya dunia. Nilipoanza msimu nililenga tu rekodi ya dunia ya 1500m kwa hivyo nashukuru Mungu kwa kupata pia ya maili moja na 5000m. Lengo langu sasa ni kutetea taji la dunia la 1500m na pia nitashiriki 5000m,” alisema.

Bingwa wa Jumuiya ya Madola 800m Moraa alisikitisha katika nafasi ya sita kwenye kitengo cha 400m alichokamilisha kwa sekunde 50.48.

Mshindi wa zamani wa Jumuiya ya Madola 800m Kinyamal alishinda mizunguko yake miwili kwa muda bora duniani mwaka huu wa dakika 1:43.22.

Kesho Jumapili ni zamu ya somo Beatrice Chepkoech (3000m kuruka viunzi na maji) na Beatrice Chebet (5000m) na Timothy Cheruiyot (1500m) kwenye London Diamond League.

  • Tags

You can share this post!

Sabina asema Uhuru anafaa kumshukuru badala ya kumlaumu

Kalonzo ajitokeza hadharani baada ya kutoonekana wakati wa...

T L