• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
Kalonzo nje ya urais, sasa kurejea Azimio wiki ijayo

Kalonzo nje ya urais, sasa kurejea Azimio wiki ijayo

NA CECIL ODONGO

KINARA wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka huenda akalazimika kurejea katika Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya baada ya jina lake kutemwa na Tume ya Uchaguzi (IEBC) kati ya wale ambao watawania urais Agosti 9, 2022.

Katika orodha iliyotolewa ya wawaniaji na tume hiyo jana, jina la Bw Musyoka halikwepo, hilo likimaanisha kuwa mwanasiasa huyo sasa hatakuwa kati ya watakaokuwa debeni.

Sababu ya Bw Musyoka kutemwa ni kuwa chama chake cha Wiper bado kiko ndani ya Muungano wa Azimio la Umoja ambao Bw Musyoka aliingia kwenye mkataba nao na kutangaza hadharani kuwa atamuunga mkono Raila Odinga miezi miwili iliyopita.

Mkataba huo unaruhusu Wiper kuondoka muungano huo baada ya Aprili 2023.

Kwenye orodha hiyo, wawaniaji 16 watamemyania Urais, nusu ya idadi hiyo ikiwa wale watakaowania kupitia vyama vya kisiasa huku wengine wanane wakiwa wagombeaji huru.

Naibu Rais Dkt William Ruto (UDA), Bw Odinga (Azimio), Ekuru Aukot (Thirdway Alliance), Mwangi Wa Iria (Usawa Party) na Njeru Gathangu (Ford Asili) na George Wajackoyah (Roots Party of Kenya), Jimi Wanjigi ni miongoni mwa wawaniaji watakaotumia vyama vya kisiasa.

Mnamo Mei 16, Bw Musyoka alitangaza kuwa ameondoka katika Azimio baada ya Bw Odinga kukosa kumtaja kama mgombeaji mwenza na kumpa waziri wa zamani Martha Karua wadhifa huo.

Badala yake, Bw Musyoka alitangaza kuwa atakuwa debeni na hata akamtaja aliyekuwa mgombeaji wa Wiper wa kiti cha Useneta katika Kaunti ya Narok Andrew Sunkuli kama mwaniaji mwenza wake.

Bw Mustoka anatarajiwa kurejea nchini wikendi hii kutoka ng’ambo na anatarajiwa kuhutubia misururu ya kampeni katika kaunti ya Narok Jumanne na Jumatano kisha kufululiza hadi ngome yake ya Ukambani wikendi ijayo.

  • Tags

You can share this post!

Nations League: Italia kualika Uingereza uwanjani San Siro...

Sonko apewa siku 21 kujibu kesi ya kutelekeza mtoto

T L