• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Sonko apewa siku 21 kujibu kesi ya kutelekeza mtoto

Sonko apewa siku 21 kujibu kesi ya kutelekeza mtoto

NA JOSEPH WANGUI

MAHAKAMA imempa makataa ya siku 21 aliyekuwa gavana wa Nairobi, Mike Mbuvi Sonko, kujibu kesi iliyowasilishwa na mwanamke anayedai kuwa mpenziwe wa zamani akisema ametelekeza jukumu la malezi ya binti yao mwenye umri wa miaka 15.

Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Ngong, Pamela Achieng, mnamo Ijumaa aliwaamuru mawakili wa Bw Sonko kujibu malalamishi hayo ili madai hayo yatengewe siku ya kusikilizwa na uamuzi kutolewa.

Korti ilitoa uamuzi huo baada ya mawakili, Mbichire & Co Advocates, kuomba kuongezewa muda ili kujiandaa kujitetea dhidi ya madai na matakwa yaliyotolewa na mwanamke huyo.

Kesi hiyo ilikuwa imetengewa siku ya kutajwa ili kuthibitisha ikiwa wakili wa mwanamke huyo alikuwa amemkabithi mwanasiasa huyo nakala za korti na ikiwa alikuwa amejibu.Wakili aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 23, 2022.

Mwanamke huyo anaitisha Sh448,450 kila mwezi kutoka kwa Bw Sonko kugharamia malezi ya mtoto ikiwemo chakula na pesa za matumizi, kodi ya nyumba, ulinzi, saluni, mavazi, mjakazi, burudani, bima ya afya, elimu, usafiri na matumizi mengineyo.

Huku uamuzi wa kesi ukisubiriwa, anamtaka Bw Sonko ashurutishwe kulipa karo ya shule ya Sh86,000 na kiasi kingine cha Sh30,450 kugharimia matumizi ya shule na sare, bima ya afya na malezi ya mtoto.

Aidha, anamtaka Bw Sonko aagizwe kulipa deni la karo la Sh37,000.

Kupitia wakili Dan Okemwa, mwanamke huyo anasema mtoto husika ni mwanafunzi wa Kidato cha Pili na bado hajarejea shule tangu zilipofunguliwa mnamo Aprili 26, 2022.

Amesema Bw Sonko ametelekeza mahitaji ya kimsingi ya mtoto huyo ikiwemo elimu, afya njema, chakula, makazi, burudani na matibabu.

“Mimi na Sonko ndio wazazi halisi wa mtoto huyu,” anasema mwanamke huyo ambaye hajatambulishwa ili kumlinda mtoto.

“Hali ya kubaguliwa imemwathiri mtoto kisaikolojia kwa sababu haelewi ni kwa nini baba yake anamchukia. Isitoshe, mtoto amedhulumiwa na kudhihakiwa shuleni kwa sababu ya jina lake hivyo kumwathiri kiakili na ameashiria kuwa anataka kuhamishwa shule hiyo,” alisema.

Anasema walikutana na Bw Sonko mnamo 1999 na punde baadaye wakaanza kuchumbiana.

Uhusiano wao ulikuwa na pandashuka hadi walipompata mtoto huyo mnamo Aprili 17, 2007.

  • Tags

You can share this post!

Kalonzo nje ya urais, sasa kurejea Azimio wiki ijayo

Wanga ajiondoa lawamani mgomo wa wahudumu

T L