• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:53 PM
Kanu yasema naibu wa Raila si lazima atoke Mlimani

Kanu yasema naibu wa Raila si lazima atoke Mlimani

NA ONYANGO K’ONYANGO

CHAMA cha KANU sasa kimejitosa katika mjadala kuhusu uteuzi wa mgombea mwenza wa mwaniaji urais kwa tikiti ya Azimio la Umoja, Raila Odinga kwa kusema kuwa, sio lazima nafasi hiyo ipewe eneo la Mlima Kenya.

Kulingana na chama hicho kinachoongozwa na Seneta wa Baringo, Gideon Moi, viongozi wa Mlima Kenya hawafai kudhani kuwa nafasi hiyo imetengewa mtu kutoka eneo lao.

“Mlima Kenya wanafaa kupigania nafasi hiyo sawa na maeneo mengine nchini. Hakuna mkataba unaosema sharti Raila ateue mtu kutoka Mlima Kenya kuwa naibu wake,” Katibu Mkuu wa Kanu Nick Salat akaambia Taifa Jumapili jana Jumamosi

Bw Odinga ambaye anaungwa mkono na zaidi ya vyama 26 chini ya muungano wa Azimio la Umoja anakabiliwa na kibarua kigumu kuteua mgombeaji mwenza wake katika kinyang’anyiro cha urais Agosti 9.

Hii imemweka katika hali tete ambayo endapo hataishughulikia kwa uangalifu huenda ikamfaidi au kumgharimu pakubwa kuelekea kinyang’anyiro hicho.

Bw Odinga anakabiliwa na utata huo wakati mpinzani wake mkuu Naibu Rais William Ruto anaendelea kuvamia ngome zake za kisiasa za 2007, 2013 na 2017.

Hata hivyo, Bw Salat anaelezea imani kuwa Bw Odinga atapata kura nyingi kutoka ngome hizo huku akipuuzilia mbali upenyo wa Dkt Ruto.

“Idadi ya kura ambayo Bw Odinga atapata kutoka eneo la Mlima Kenya itakuwa ni bonasi tu. Kura za Raila zingalipo ilivyokuwa katika chaguzi za 2007, 2013 na 2017,” akasema.

Bw Salat pia anasema Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta hawafai kuwekewa presha kuhusu nafasi ya mgombea mwenza.

“Tunahitaji asilimia 40 za kura kutoka eneo la kati mwa Kenya kushinda katika uchaguzi wa urais,” akaongeza.

Kauli ya Bw Salat inajiri siku chache baada ya naibu mwenyekiti wa Jubilee, David Murathe kudai kuwa, Bw Odinga anaweza kushinda urais hata bila kura za Mlima Kenya.

Bw Murathe ambaye alikuwa akiongea katika kipindi cha mahojiano katika runinga moja ya humu nchini alisema nusra Bw Odinga ashinde katika chaguzi za 2013 na 2017 bila uungwaji mkono kutoka Mlima Kenya.

 

  • Tags

You can share this post!

Uhispania yasubiri hadi dakika ya mwisho kuzamisha Albania...

Kibicho, Ndiritu wazozana kuhusu vituo vya polisi

T L