• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Kesi zaumiza raia

Kesi zaumiza raia

NA WAANDISHI WETU

IDADI ya viongozi wanaoandamwa kwa madai ya ufisadi inazidi kuongezeka na kuwaacha wananchi bila uongozi mwafaka, uwakilishi na huduma kutatizika.

Hii ni kutokana na viongozi wa kisiasa wakiwemo magavana na wabunge kutumia muda mwingi na rasilimali kujaribu kujinasua kutoka katika meno makali ya sheria, muda ambao wanafaa kutumia kuhudumia wananchi.

Wakazi wa eneobunge la Sirisia katika Kaunti ya Bungoma kwa wakati huu hawana uwakilishi bungeni baada ya mbunge wao John Waluke kufungwa gerezani kwa uporaji mnamo Juni.

Gavana wa Migori Okoth Obado jana alijiunga na orodha ya wanasiasa wanaokabiliwa na kesi kwa tuhuma za kuipora kaunti hiyo zaidi ya Sh73 milioni.

Mahakama ilimwagiza Bw Obado kutofika afisini mwake hadi pale kesi hiyo itakapomaliza kusikizwa na kuamuliwa, hivyo kumaanisha utendakazi wake kwa wakazi wa Migori utatatizika

Bw Obado na wanawe wanne waliachiliwa kwa dhamana ya jumla ya Sh18.3 milioni na Mahakama ya Milimani.

Hapo jana pia, Mbunge wa Malindi, Aisha Jumwa alikanusha mashtaka sita ya ufisadi dhidi yake katika mahakama ya kushughulikia kesi za ufisadi jijini Mombasa.

Bi Jumwa anakabiliwa na mashtaka ya wizi wa Sh19 milioni kutoka kwa Hazina ya Maendeleo ya eneobunge la Malindi (NG-CDF).

Hakimu mkuu wa Mombasa, Edna Nyaloti, alimwachilia Bi Jumwa kwa dhamana ya Sh5 milioni na mdhamini wa kiasi sawa hicho au Sh2 milioni pesa taslimu.

Jana, kesi dhidi ya aliyekuwa gavana wa Kiambu, Ferdinard Waititu ilikosa kuanza katika Mahakama Milimani ya Kushughulikia Kesi za Ufisadi baada ya mshtakiwa kukosa kufika mahakamani.

Bw Waititu anakabiliwa na tuhuma za kuipora kaunti hiyo Sh510 milioni.

Wakili wake, John Swaka, aliiambia mahakama kwamba Bw Waititu ameambukizwa virusi vya corona, hivyo hangeweza kufika kortini. Bw Waititu alikuwa ameachiliwa kwa dhamana ya Sh30 milioni.

Kesi yake ilisababisha mgogoro katika Kaunti ya Kiambu hasa korti ilipoamuru asiingie afisini hadi kesi ikamilike, hali iliyovuruga usimamizi na utoaji huduma hadi alipoondolewa ofisini na Seneti.

Viongozi wengine wanaokabiliwa na kesi za ufisadi ni magavana Mike Sonko (Nairobi), Sospeter Ojaamong (Busia) na Moses Lenolkulal wa Samburu.

Bw Sonko aliachiliwa kwa dhamana ya Sh15 milioni pesa taslimu, na kuagizwa kutoingia katika afisi yake.

Madai hayo ya ufisadi yamekuwa kigezo cha baadhi ya madiwani katika kaunti hiyo kutaka atimuliwe, hali ambayo imeibua mivutano kwa muda mrefu na kutatiza utoaji huduma kwa wananchi.

Bw Ojaamong naye anakabiliwa na shtaka la kuipora kaunti ya Busia Sh8 milioni ambapo tayari mahakama imeamua ana kesi ya kujibu.

Kando na viongozi walioshtakiwa, asasi za kupambana na ufisadi ikiwemo Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), Idara ya Mashtaka ya Umma (DPP) na ile ya kuchunguza uhalifu (DCI) zinachunguza wengine wengi ambao huenda wakashtakiwa hivi karibuni.

Hawa ni pamoja na Gavana Anne Waiguru wa Kirinyaga ambaye anachunguzwa na EACC kwa tuhuma za kujifaidi kwa Sh10.6 milioni kama marupurupu ya usafiri.

Mapema mwezi huu EACC ilisema inafuatilia madai ya ufujaji wa Sh31.4 milioni dhidi ya Gavana Hassan Joho wa Mombasa, huku Mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohamed naye akimulikwa kuhusu uporaji wa Sh129 milioni za NYS

Ripoti za Wanderi Kamau, Joseph Wangui, Richard Munguti na Philip Muyanga

You can share this post!

Matakwa ya wazazi kabla ya shule kufunguliwa

Rais akiri corona ilimchanganya sana