• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 5:50 AM
Kibarua cha Raila kulinda ufuasi Gusii

Kibarua cha Raila kulinda ufuasi Gusii

NA DAVID MWERE

KIONGOZI wa muungano wa Azimio Raila Odinga anakabiliwa na kibarua cha kudumisha ushawishi wake wa kisiasa katika eneo la Gusii kufuatia hatua ya Rais William Ruto kujaribu kutwaa ngome hiyo kupitia teuzi serikalini.

Tayari Rais Ruto amempendekeza Mbunge wa zamani wa Nyaribari Masaba Ezekiel Machogu kuwa Waziri wa Elimu na Mbunge wa Mugirango Kusini Sylvanus Osoro kuwa kiranja wa wengi katika bunge la kitaifa.

Uteuzi wa Mbw Machogu na Osoro unafasiriwa kama mpango wa Rais Ruto unaolenga kufurahisha jamii hiyo ili kuiondoa kisiasa, kutoka udhibiti wa Bw Odinga.

Kiongozi huyo wa ODM amekuwa akivuna kura nyingi za urais kutoka eneo la Gusii katika chaguzi zilizopita.

Sasa Bw Odinga sharti “arudishe mkono” kwa kuwatunuku wabunge kadha kutoka eneo hilo nafasi katika kamati za bunge, Tume ya Huduma za Bunge (PSC) na Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA).

Hii ni baada ya wabunge kutoka kaunti za Kisii na Nyamira kukosa kupewa nafasi katika safu ya juu ya uongozi wa Azimio katika Bunge la Kitaifa na Seneti.

Juzi, Azimio ilimteua Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi (ODM) kuwa kiongozi wa wengi katika Bunge la Kitaifa huku Mbunge wa Kathiani Robert Mbui (Wiper), akiteuliwa naibu wake.

Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed (ODM) aliteuliwa kiranja wa wengi na Mbunge Maalum Sabina Chege (Jubilee) akateuliwa naibu wake.

Katika Seneti, Seneta wa Kilifi Stewart Madzayo (ODM) aliteuliwa kiongozi wa wachache huku mwenzake wa Kitui Enoch Wambua (Wiper) akiteuliwa naibu wake.

Seneta wa Isiolo Fatuma Dullo (Jubilee) aliteuliwa kiranja wa wachache huku seneta wa Nairobi Edwin Sifuna akiwa naibu wake.

Hii ina maana kuwa nafasi aliyonayo Bw Odinga kuzawadi eneo la Gusii na maeneo mengine yaliyosalia, ni kupitia teuzi katika kamati zenye hadhi ya bunge, PSC na EALA.

Kuna nafasi tisa katika bunge hilo lenye makao yake Arusha, Tanzania ambazo zitagawanywa kati ya ODM na chama cha United Democratic Alliance (UDA) chake Rais Ruto.

Hii ni kwa sababu vyama hivyo ndivyo vina idadi kubwa ya wajumbe katika Bunge la Kitaifa na Seneti.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, Bw Amos Nyasani, anasema kuwa ikiwa Bw Odinga anataka kuendelea kuwa na ushawishi wa kisiasa katika eneo la Gusii, anafaa kuteua watu kutoka maeneo hayo katika kamati za PSC na EALA.

“Pia Bw Odinga anafaa kuteua wabunge wa kutoka Gusii katika kamati za bunge kuhusu uhasibu (PAC) na ile ya uwekezaji (PIC). Pia ahakikishe baadhi yao wameteuliwa katika bunge la EALA na tume ya PSC,” anasema Bw Nyasani.

“Ikiwa Bw Odinga atapuuza eneo la Gusii, Rais Ruto ataponyoka eneo hilo,” akaongeza.

Tayari Seneta wa Nyamira Okong’o Omogeni na mwenzake wa Homa Bay Moses Kajwang’ wanang’ang’ania idhini ya ODM kuwakilisha seneti katika tume ya PSC.

  • Tags

You can share this post!

Kaunti za eneo la Ziwani kuelimisha jamii kuhusu Ebola

Mpira wa Vikapu: Kenya yaambulia patupu mashindano ya Red...

T L