• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 5:50 AM
Kibicho ataka UDA iwakome machifu

Kibicho ataka UDA iwakome machifu

NA KENYA NEWS AGENCY

KATIBU katika Wizara ya Usalama Karanja Kibicho amewataka viongozi wa Kenya Kwanza kukubali kuwa mkondo wa siasa umebadilika na wakome kuilaumu serikali.

Dkt Kibicho alidai chama cha United Democratic Alliance (UDA) ambacho ni mojawapo ya vyama tanzu katika muungano huo kimewahadaa Wakenya tangu 2018, lakini sasa raia wamegundua uwongo wao.

“Ni uwongo kwa viongozi wa UDA na Kenya Kwanza kudai kuwa machifu na manaibu wao wanatumiwa katika siasa. Hawa ni maafisa wa serikali ambao hawapaswi kuwashawishi wapiga kura,” akasema Jumamosi katika Shule ya Msingi ya Gathaka, kaunti ndogo ya Kirinyaga Magharibi, kaunti ya Kirinyaga.

“Tangu 2018 viongozi wa UDA wamekuwa wakizunguka nchini wakieneza uwongo huku wakitoa uhadi nyingi. Lakini sasa Wakenya wamegundua kuwa wamekuwa wakidanganywa na ndio maana wamebadili misimamo yao,” Dkt Kibicho akaongeza.

Katibu huyo aliwatetea machifu ambao wamekuwa wakikashifiwa na viongozi wa UDA kwamba wanasambaza chakula cha msaada kwa familia zinazoathiriwa na njaa, ili kuzishawishi kisiasa.

Akasema Dkt Kibicho: “Tangu zamani machifu wamekuwa wakitumika na serikali zilizopita katika mpango wa usambazaji wa chakula cha msaada. Na UDA ikishinda uchaguzi wao pia watawatumia machifu kusambaza chakula cha msaada kwa sababu wao ndio wanawafahamu wafahamu watu wao.”

Dkt Kibicho pia aliapa kuendelea kuwafundisha raia kuhusu haja ya kuwachagua viongozi wasio na doa la ufisadi. Dkt Kibicho, ambaye ni mwanafunzi wa zamani wa shule hiyo, alisema taifa hili linafaa kuongozwa na wanaume na wanawake wenye maadili.

“Wale ambao wanayo maadili ya kutiliwa shaka hawafai kupewa nafasi ya uongozi.”

“Hili ni taifa lenye utajiri mkubwa wa viongozi bora na nitajizatiti kuhakikisha kuwa ni viongozi wenye sifa nzuri ndio wanapewa nafasi ya uongozi,” akasema.

Kauli sawa na hiyo ilitolewa na Askofu wa Kanisa la Kianglikana (ACK) eneo hilo, Joseph Kibucwa ambaye aliwaonya wapiga kura dhidi ya kukubali kuhongwa ili kupigia kura wagombeaji .

Askofu huyo nyakati nyingi ameonya wakazi dhidi ya kupiga kura kwa mfumo wa suti akisema utachangia kuchaguliwa kwa viongozi wasiofaa.

“Kama Kanisa tunapinga mfumo wa upigaji kura wa ‘six piece’ unaochochewa na msisimko wa vyama. Hii ni kwa sababu hali hii huweza kuchangia kuchaguliwa kwa viongozi wasio na maadili wala sifa hitajika za uongozi,” Askofu Kibucwa akasema.

  • Tags

You can share this post!

Paul Pogba arejea Juventus baada ya kuondoka Man-United

Chakula: Magoha awapa matumaini walimu wakuu

T L